Wanasiasa Waliowagusa Wananchi Mwaka 2021 Mkoani Manyara

Kwa mwaka 2021 ambao unaenda ukingoni yapo mambo mengi ambayo yamefanywa na viongozi wa kisiasa katika mkoa wa Manyara.

JIMBO LA BABATI MJINI
Tukianza kabisa na Mbunge wa jimbo la Babati mjini ambaye pia ni Naibu waziri wa Sanaa,Utamaduni na Michezo Paulina Philip Gekul, kwenye sekta ya afya alihakikisha unafanyika ujenzi wa wodi ya Mama na mtoto katika hospitali ya mji wa Babati (Mrara) na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Afya Sigino.

Katika upande wa Elimu Mheshimiwa Paulina Gekul aligawa mashine za kutolea nakala (Photocopy Machine) katika shule tano za Sekondari huku zaidi ya shilingi Milioni 28 zikitumika katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo jimboni hapo.

Alifanya kwa vitendo kazi yake ambapo katika jimbo alianzisha ligi ya Jimbo iliyogusa Michezo aina yote ikishirikisha wanaume na wanawake.
Michezo hiyo iliwaleta watu karibu na kuwafanya vijana kuwa bize na michezo na kuacha kukaa vijiweni.
JIMBO LA HANANG
Mbunge wa kundi la Vijana ambaye anatokea katika kata ya Endasak wilayani Hanang mkoa wa Manyara Asia amekuwa akifanya jitihada mbalimbali kuwahamasisha vijana kujiunga kwenye vikundi ili waweze kukopesheka na kujikwamua kimaisha kwa kufanya shughuli mbalimbali za uzalishaji.Amekuwa akishiriki shughuli mbalimbali za kijamii na hata muda mwingine kutoa fedha zake mfukoni katika harambee kwenye nyumba za ibada.
Katika Uchaguzi ujao Mbunge huyo anaonekana dhahiri kuwa analihitaji Jimbo hilo la Hanang linaloongozwa na Mhandisi Samwel Hayyuma.

BABATI VIJIJINI
Jimbo hilo linaongozwa na Mchumi Daniel Baran Sillo ambaye katika muda wake wa uongozi hadi sasa ameweza kuwakumbuka wananchi kwa kufanya vikao mbalimbali na kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili ambapo ameweza kutembelea kata zote 25 za jimbo hilo lenye vijiji 102.
Aliingia madarakani Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 akimshinda kwa kura za Maoni aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo Vrjilal Jituson.

Mheshimiwa Daniel Sillo kwa upande wa Afya katika Vijiji vya Ayasanda,Guse na Ayamango alipeleka shilingi Milioni 50 kwa kila Zahanati ambazo zipo katika hatua mbalimbali za kukamilika, na kwa sasa wameanza ujenzi wa wa vituo vitatu vya kutolea huduma ya afya Ayasanda,Bashnet na Madunga.
Kwa upande wa Elimu katika jimbo la Babati Vijijini kulikuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa 45 vya shule za sekondari lakini kwa jitihada za Mbunge huyo yamepatikana madarasa 78 hadi sasa wakati mwaka 2021 unamalizika.

Kwa upande wa Miradi ya Maendeleo iliyochangiwa kupitia Mfuko wa kuchochea maendeleo ya Jimbo Jumla ya fedha shilingi Milioni 25,270,541 zilitumika katika kukarabati Miundo mbinu ya shule ambapo yalinunuliwa mabati 1,053 na mifuko 1,765 ya saruji.
JIMBO LA KITETO
Jimbo hilo linaongozwa na wakili Msomi Edward Ole Lekaita, aligusa nyanja mbalimbali ambapo katika afya na Elimu, zaidi ya shilingi Milioni 67 za mfuko wa jimbo zimelenga kuboresha sekta hizo.
Wananchi wa Jimbo la Kiteto katika kuendesha maisha yao shughuli zao ni Kilimo na Ufugaji ambapo Mbunge Ole Lekaita katika kuhakikisha wakulima wanalima kwa tija, alitembelea makundi mbalimbali ya wakulima na kuwashauri juu ya kilimo bora na utumiaji wa mbegu za kisasa.
Katika Michezo Mheshimiwa Ole Lekaita hakubaki nyuma,aliweza kutoa mipira kwa kata zote za wilaya ya Kiteto ambapo timu za mpira wa miguu zaidi ya 32 zimenufaika.

Na John Walter-Manyara

Post a Comment

0 Comments