Wanaume hunyanyaswa ila wagumu kusema

Ukizungumza unyanyasaji wa kijinsia wengi huwaza wa upande mmoja, kwamba ni dhidi ya mwanamke lakini uhalisia ni tofauti kwani hata wanaume hunyanyaswa isipokuwa si wepesi kuzungumza.

Hayo yalielezwa mapema wiki hii wakati wa kongamano la kupinga ukatili wa kijinsia lilioandaliwa na Norwegian Church Aid (NCA) mkoani Manyara ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya simu 16 za kupinga ukatili wa Kijinsia, kauli mbiu ni “Ewe Mwananchi Komesha Ukatili wa Kijinsia Sasa”

Katika kongamano hilo lililohudhuriwa na viongozi wa dini, wanaharakati, wazee wa mili na viongozi wa Serikali Mwakilishi wa kamanda wa polisi mkoani humo ACP Yahaya Athumani alisema hata wanaume hunyanyaswa isipokuwa hawasemi.

“Katika kupambana na unyanyasaji wa kijinsia jeshi la polisi limeanzisha madawati ya jinsia, wakati tunatafakari kuhusu jambo hilo tusifikiri ni la watoto na wanawake tu, hata wanaume wapo wanaogopa tu kufunguka, sisi tunashuhudia mengi huko kwenye madawati ndiyo maana nasema tuangazie pande zote,” amesema Athumani.

Afisa maendeleo ya jamii wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto, Regina Mollel amesema hakuna takwimu za unyanyasaji wa kijinsia kwa wanaume kama ilivyo kwa wanawake na watoto lakini kuna visa vya wanaume kupigwa na wenza wao katika maeneo mbalimbali jambo ambalo nalo ni unyanyasaji.

“Wanaume wameumbwa kujisimamia lakini wakati mwingine wanapigwa, takwimu hamna lakini wapo wanaonyanyaswa na wakiwa walemavu ndo kabisaa,” amesema Mollel aliyemwakilisha katibu mkuu wa Wizara katika mkutano huo.

Amesema tatizo wanaume hawasemi lakini wapo wanaonyanyaswa lakini wanawake wanasemwa zaidi kwa kuwa ukatili kwao umekithiri hivyo kupinga ukatili kwa ujumla wake ni jambo ambalo linahitaji jitihada za pamoja.

Mkurugenzi Mkazi wa NCA nchini, Pauliina Parhiala amesema unyanyasaji ni uvunjifu wa haki za binadamu, ni uhalifu, lakini pia ni makosa ya kimaadili, hakuna faida yoyote zaidi ya madhara ya muda mfupi na muda mrefu.

“Kwa mtu binafsi ukatili husababisha mshtuko wa kihisia, majeraha ya kimwili, magonjwa ya zinaa, udumavu, matatizo ya afya ya uzazi, mimba zizizotarajiwa hata kifo,” amesema Parhiala.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments