Recent-Post

Wanawake wamshambulia mkandarasi Bariadi, atimua mbio


 Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu linawashikilia wanawake wanne kwa tuhuma za kumshambulia mkandarasi anayejenga barabara ya Nkololo Bariadi wakati wakifanya mila ya 'Pumbulu'.

Taarifa iliyotolewa leo Desemba 14, 2021 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Blasius Chatanda imesema kuwa kundi la wanawake lilimshambulia mkandarasi (hakutaja jina) kwa kumpiga na mawe sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia majeraha.

Amesema kundi hilo la wanawake walikuwa katika kutimiza mila zao za Kisukuma, ambapo mwanamke amejifungua na ikatokea mtoto amefariki huwa wanaenda kufanya tambiko hivyo wakiwa njiani wakikutana na mwanaume yoyote wanaanza kumshambulia.

Taarifa hiyo ya Kamanda Chatanda imesema kuwa baada ya mkandarasi huyo kushambuliwa alikimbia ili kuwakwepa wanawake hao.

Amesema kuwa watuhumiwa hao wapo nje kwa dhamana na mara baada ya upelelezi kukamilika watafikishwa mahakamani.

Kamanda Chatanda ametoa wito kwa wananchi kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi mila hizo isiwe chanzo cha kujichukulia sheria mkononi.

Mila ya Pumbulu

Mwenyeji wa Mkoa wa Simiyu, Constantine Mathias meielezea mila ya Pumbulu kuwa huwa inatokea mara moja kwa muda mrefu na kuwa mila hiyo inahusisha wanawake pekee.

Amsema "Mtoto akifariki punde mara baada ya kuzaliwa katika jamii ya kabila la Wasukuma inachukuliwa kama ni mkosi hivyo kuondoa mkosi huo ndipo wanawake wa kimila wanafanya tambiko" amesema Constantine.

Amesema tambiko hilo linahusisha kuvunja vyungu na vitu vingine vinavyo husishwa na tambiko hilo ili kuondoa mkosi kwenye jamii baada ya kuvunja hubeba mabaki yaliyosalia kisha kutembea umbali mrefu kwenda kutupa mabaki hayo.

Baada ya kuwa wametupa aidha njiapanda au barabarani wanawake wa eneo husika watayachukua mabaki hayo na kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kuyatupa.

"Huwa linakuwa ni zoezi endelevu ambapo kila mabaki hayo yanapotupwa wanawake wanayachukua kuyatupa hadi yatakapo fika ziwani ambako ndipo huwa wanakusudia kuutupa mkosi huo" amesama

Ameongeza kuwa wakati wa utekelezaji wa mila hiyo kundi kubwa la wanawake huandamana kwenda kutimiza mila hivyo katika maandamano hayo haipaswi kukutana na mwanamme yeyote wanapokuwa njiani.

"Ikitokea wakakutana na mwanaume au akakatiza mwanaume katika msafara wao humshambulia na kumpiga au kumvua nguo"

Amesema tangu kutokea kwa tukio la mkandarasi kupigwa Desemba 9, 2021 maeneo ya kata ya Nkololo wilayani Bariadi mabaki hayo yanazidi kusafirishwa kwa mtindo ule ule na yamefika kata ya Ngulyati wilaya ya Bariadi na yataendelea kusafirishwa hadi yatakapofika ziwani.

Post a Comment

0 Comments