Yanga chini ya matajiri mambo mazito yaja, Senzo afunguka yote


WANACHAMA na mashabiki wa Yanga, sasa wajiandae tu kutembea kifua mbele, kwani mambo yao yameanza kunoga kuelekea kwenye mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji na kwa sasa ni suala la muda kabla ya klabu hiyo kuendeshwa kishua ikiwa mikononi mwa matajiri wasiopungua watatu wakaowekeza fedha zao Jangwani.

Kama hujui ni kwamba Yanga ilikamilisha usajili wa Katiba Mpya, baada ya wanachama kupitisha rasimu ya katiba ya mabadiliko ya klabu hiyo katika mkutano mkuu uliofanyika Juni 27 wakiongozwa na Rais wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Kikwete jijini Dar es Salaam.

Baada ya miezi kadhaa kupita, juzi klabu hiyo imekabidhiwa rasmi katiba hiyo ambayo imepitishwa na msajili wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Desemba 14.

“Kinachofuata sasa ni kuelekea kwenye mchakato wa kufungua kampuni, kuthaminisha mali za klabu na mambo mengine yanayotakiwa kufuata kwa ajili ya kuanzisha kampuni,” alisema Kaimu Mtendaji Mkuu Yanga, Senzo Mazingisa.

Kaimu Msajili wa BMT, Patrick Kipangula aliye pia ni msajili wa magazeti alisema katiba ya Yanga ilishapitishwa, ingawa hana uhakika kama klabu hiyo imeshakwenda kuichukua BMT.

“Siko ofisini, lakini ukiwauliza Yanga wenyewe watakujibu kuhusu hili,” alisema msajili.

Hata hivyo, Senzo sambamba na kiongozi mwingine wa juu aliyeomba kuhifadhiwa jina, alisema tayari klabu imeshakabidhiwa katiba yao tangu Desemba 15, hivyo wakati wowote kuanzia sasa mchakato wa mabadiliko utaendelea.

“Tulichokuwa tunakisubiri ilikuwa ni katiba kupitishwa ili mambo mengine yafuate, sasa tuna baraka zote za kuendelea na mchakato huu ambao kwa mujibu wa katiba yetu mpya, wawekezaji wataanzia watatu,” alisema.

Kwa mijibu wa katiba hiyo ni kwamba matajiri wasiopungua watatu wanaoweza kuwekeza watakuwa na hisa za asilimia 49 na nyingine 51 zilizobaki zitamilikiwa na wanachama wa klabu hiyo, kwa vile sasa Yanga itakuwa kama kampuni.

Mapema wakati wa mchakato ukianza, kulikuwa na majina matatu yaliyowapagawisha wanayanga juu na mabadiliko hayo wakiamini wakitua tu, klabu yao itakuwa kama klabu nyingine za kisasa zitakazokuwa na uwezo wa kujiendesha kiuchumi bila kutegemea mifuko ya watu.

Mabilionea hao waliokuwa wakipigiwa chapuo ni Ghalib Said Mohammed ‘GSM’ ambaye kampuni yake kwa sasa inaidhamini Yanga na kumwaga fedha nyingi kufanya usajili ya kibabe na pia kuijenga timu kuwa ya ushindani baada ya misimu kadhaa kuwa ovyo sana.

Pia yupo aliyekuwa Mwenyekiti na mfadhili wao mkubwa, Yusuf Manji ambaye siku ya mkutano wa kupitisha katiba hiyo aliibuka ukumbini na kuwadatisha wanachama waliomshangilia na mtu wa mwisho ni bilionea mwingine wenye fedha zake, Rostam Aziz.

Katika mabadiliko ya katiba, kati ya vipengele ambavyo vilipitishwa na wanachama ni kile cha Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo kuongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Yanga Sports Club Company Limited (YASCCL).

Watakaokuwa chini yake ni kitengo cha fedha, utawala na sheria, kitengo cha rasilimali watu (HR) na kitengo cha ‘commercial and marketing’ ambavyo pia vitakuwa na watu walio chini yake.

“Safari ndiyo imeanza rasmi, wakati wowote kuanzia sasa safari ya mabadiliko itatangazwa kwa mchakato kuendelea,” alisema Senzo.

Yanga inaenda kujiendesha kwa mfumo wa hisa kama ilivyofanya kwa watani wao wa jadi Simba iliyo chini ya Mohammed Dewji aliyeweka mzigo wa Sh 20 bilioni katika asilimia 49 anazomiliki na asilimia iliyosalia itabaki kwa klabu chini ya wanachama wake.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments