Recent-Post

Zitto amtaja Mbowe miaka 60 ya uhuru


 Kiongozi wa ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe ameshauri kufanyika kwa mambo manne, likiwemo suala la Freeman Mbowe, ili kuikamilisha furaha ya Watanzania na hatua kubwa ya mafanikio iliyopigwa katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru.

Katika salamu zake alizotoa kupitia hotuba yake kwa Taifa aliyoirusha moja kwa moja kupitia mitandao ya kijamii, Zitto (pichani) alisema ipo haja ya kufanyika mazungumzo ya viongozi wa vyama vya siasa ili kutafakari na kurekebisha makosa makubwa ya 2019 na 2020.

Jambo la pili ni ili kufanikisha mazungumzo hayo, mashtaka yanayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe yaangaliwe upya akidai suluhisho la tuhuma zake lazima liwe la kisiasa si la kijinai.

“Nazisihi mamlaka zinazohusika na mashtaka kuwa Mbowe aachiwe huru ili tuwe naye kwenye mazungumzo kati ya Rais na vyama vya siasa mnamo Desemba 16 - 17, 2021,” alisema Zitto.

Hoja kama hiyo vilevile ilitolewa juzi na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia katika moja ya midahalo ya uhuru, akimtaka Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) afute kesi hiyo kwa madai haina masilahi kwa nchi.

Lingine aliloshauri ni kuhusu mazungumzo ya vyama vya siasa akitaka yajikite kwenye kuangalia namna nzuri ya kuandika upya Sheria ya Uchaguzi na Sheria ya Vyama vya Siasa sambamba na kutazamwa upya na kufanyiwa marejeo sheria mbalimbali kandamizi.

Zitto pia alishauri kuanza kwa majadiliano na mazungumzo rasmi ya kitaifa kuhusu namna ya kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya.

Alisema: “Mwaka 2022 tunatimiza miaka 30 tangu nchi yetu irejee kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa. Ni muhimu sasa kuanza majadiliano na mazungumzo rasmi kitaifa kuhusu namna ya kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya”.

Alisema katika miaka 60 ya uhuru nchi bado inakabiliwa na changamoto kadhaa, mbaya zaidi zikiwa ni zile ambazo zipo ndani ya uwezo wetu, hasa zile zinazovunja umoja wa kitaifa.

“Kwa hakika hatuko wamoja, kuna manung’uniko mengi, hasa ya kisiasa na hata kiuchumi. Tuna miaka 60 ya uhuru lakini bado hatuna uhuru na ustaarabu wa kuchagua viongozi wetu kwa haki, tukiitisha uchaguzi ni lazima tuuane.

“Tuna miaka 60 lakini hatuvumiliani kisiasa, tunashutumiana na hata kufungana, tunazuiana kufanya shughuli halali za kisiasa, tuna miaka 60 lakini bado tu maskini,” alisema Zitto.

Akizungumzia miaka 60 ijayo, Zitto alisema, “ningetamani miaka 60 ijayo, Taifa letu liendelee kuwa moja, lenye ushawishi kwenye ukanda huu na duniani kwa ujumla. Taifa lenye wananchi wanaojitambua, wenye maarifa, wasio maskini na wanaopendana.

“Bila kuwa wamoja sasa, hatutaweza kukaa pamoja na kujenga hilo ninalotamani kurithisha kwa vizazi vinavyokuja. Lakini ili kuwa wamoja ni lazima tuimarishe mifumo ya haki ili kudumisha amani. Tusiogope kujadiliana,” alisema kiongozi huyo.

Post a Comment

0 Comments