Aliyemtishia Nape bastola kizimbani

Maofisa saba wa Jeshi la Polisi wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Hakimu Mkazi Mtwara, kwa tuhuma ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis aliyekuwa akiishi Nachingwea mkoani Mtwara.

Miongoni mwa washtakiwa hao ni Gilbert Kalanje, ambaye aliwahi kumtolea bastola Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia, Nape Nnauye.

Tukio la Nape kutishiwa kwa bastola lilitokea Machi 23, 2017, baada ya mwanasiasa huyo kutenguliwa katika wadhifa wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, alipokuwa akijiandaa kufanya mkutano na waandishi wa habari katika Hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam, lakini baadhi ya askari kanzu, akiwamo Kalanje aliyemtolea bastola walimzuia.

Maofisa wengine waliotajwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Mark Njera ni aliyekuwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtwara, Mrakibu Msaidizi wa Polisi Charles Onyango, aliyekuwa Mkuu wa Intelijensia Mkoa, Mrakibu wa Polisi, Bicolas Kisinza, Mkaguzi wa Polisi, John Msuya, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Marco Mbota, Mkaguzi wa Polisi, Shiraz Ally Mkuka na G5158, Koplo Salum Juma Mbalu.

Akizungumza na Mwananchi jana, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Lugano Kasebele alisema washtakiwa walifikishwa mbele yake na kusomewa mashtaka, lakini hawakutakiwa kujibu chochote.

“Upelelezi bado haujakamilika, hivyo kesi hiyo itatajwa tena Februari 8, 2022. Upelelezi utakapokamilika kesi hiyo itapelekwa Mahakama Kuu Kanda ya Kusini kwa ajili ya kusikilizwa,” alisema Hakimu Kasebele.

Aliongeza kuwa kwa kuwa shtaka walilosomewa halina dhamana, washtakiwa hao wamepelekwa rumande katika gereza la Lilungu lililopo wilayani Mtwara.

Mwendesha mashtaka wa kesi hiyo ni Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wilbroad Ndunguru.

Hata hivyo, miongoni mwa maofisa wanaotuhumiwa kuhusika na tukio hilo, alikuwa Grayson Mahembe anayedaiwa kujinyonga hadi kufa akiwa mahabusu, jambo lililozua maswali kuhusu uwezekano huo huku familia yake ikitaka kufanyika kwa uchunguzi wa kina ili haki iweze kutendeka.


Usalama wa mahabusu

Akizungumzia suala hilo alipoulizwa na Mwananchi kwa simu jana, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime alisema licha ya ofisa huyo kufariki dunia, bado mahabusu za polisi nchini zina usalama.

“Ni kwamba selo au mahabusu za polisi zinajengwa katika hali ya kuzingatia masuala ya kiusalama ya kuhakikisha wanaoingizwa mle wanakuwa salama saa zote. Ndiyo maana wanaingizwa watuhumiwa maelfu Tanzania nzima na wote wanatoka wakiwa salama.

“Linapotokea tukio moja huwezi kuhitimisha kwa kusema kuwa mahabusu hizo haziko salama,” alisema Misime.

Akifafanua zaidi, Misime alisema; “Tukumbuke anayeingizwa mle wakati mwingine anapo tafakari kosa alilotenda na kuona ushahidi ulivyo mzito dhidi yake na ni aibu kwake, anashindwa kuhimili au kuvumilia hali hiyo na ndipo huanza kutafuta mbinu za kujidhuru, ikiwapo ya kujinyonga au hata kutoroka.

“Pia tukumbuke huyo ni binadamu, anayo maarifa mengi ya kufanya alilokusudia akipata mazingira mazuri kama vile mahabusu wenzake wanapokuwa wamelala. Jeshi la polisi linaendelea kusisitiza kuwa selo au mahabusu katika vituo vya polisi ni salama,” alisema Misime.

Alipoulizwa kuhusu uchunguzi wa mwili wa Mahembe kabla hajazikwa mkoani Iringa, Misime alisema kwa mtu aliyekufa katika mazingira hayo, ni lazima taratibu zote za kisheria zifuatwe.

“Ikiwepo kuufanyia mwili uchunguzi wa kitaalamu ambayo kama ulivyosema kuufanyia mwili postmortem kwa sababu inafahamika fika lazima hilo litaulizwa,” alisema Misime.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments