Ethiopia yatangaza msamaha kwa wafungwa wa kisiasa akiwemo kiongozi wa upinzani

Serikali ya Ethiopia imetangaza kuwa itatoa msamaha na kuwaachia huru wafungwa mashuhuri wa kisiasa akiwemo kiongozi wa upinzani Jawar Mohammed na maafisa wa chama cha upinzani cha Tigray.

Tangazo hilo limetolewa baada ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed kutoa taarifa ya mwito wa kutafuta "maridhiano ya kitaifa" huku nchi hiyo ikisherehekea Krismasi ya madhehebu ya Othodoksi.

Orodha ya wanasiasa watakaopewa msamaha ni pamoja na wanachama kadhaa waandamizi wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF), ambao wapiganaji wao wamekuwa kwenye vita na mapigano makali na vikosi vya jeshi la serikali ya Addis Ababa tangu Novemba 2020, pamoja na viongozi mashuhuri wa upinzani kutoka jamii za Oromo na Amhara.

Hata hivyo bado haijafahamika ni wangapi kati ya waliopewa msamaha huo tayari wameshaachiwa huru.

Uamuzi huo unaonekana kama hatua ya ghafla na ya kushtukiza zaidi kuchukuliwa na serikali, baada ya vita vikali vilivyoikumba Ethiopia vya Tigray kuingia kwenye hatua mpya mwishoni mwa Desemba wakati vikosi vya eneo hilo vilipoamua kurudi nyuma huku vile vya serikali navyo vikitangaza kuwa havitasonga mbele zaidi ya pale vilipofikia.

Jawar Mohammed
                    
Shirika la Utangazaji la Ethiopia EBC limemtaja Jawar Mohammed na Eskinder Nega, ambao walikamatwa na kuwekwa kizuizini Julai 2020 kufuatia machafuko makubwa yaliyozuka baada ya kuuawa msanii maarufu wa jamii ya Oromo Hachalu Hundessa, kuwa ni miongoni mwa wanasiasa waliopata msamaha huo wa serikali.

Sebhat Nega, Kidusan Nega, Abay Woldu, Abadi Zemu, Mulu Gebregziabher na Kiros Hagos ni miongoni mwa viongozi wa Tigray waliopewa msamaha na kusisitizwa kuwa wataachiwa huru hivi karibuni.

Wizara ya Sheria ya Ethiopia imesema, msamaha kwa Mohammed Jawar na Eskinder Nega umetolewa ili "mazungumzo yajayo ya kitaifa yafanikiwe na yawe jumuishi"

Desemba 29, wabunge wa Ethopia walipitisha mswada wa kuundwa tume ya mazungumzo ya kitaifa, wakati nchi hiyo ikiandamwa na mashinikizo ya kimataifa ya kuitaka ianzishe mazungumzo ya kuhitimisha vita

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments