Recent-Post

HALMASHAURI 9 KIKAANGONI UKUSANYAJI MAPATO KIDUCHU

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa,akizungumza  na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu mapato na matumizi ya ndani ya halmashauri kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba.

………………………………………………………….

Na.Alex Sonna,Dodoma

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa ameziweka kikaangoni halmashauri 9 ambazo zimekusanya chini ya asilimia 50 ya lengo la mwaka la makusanyo ya ndani.

Pia  amezitaka halmashauri hizo kuwasilisha maelezo kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, kuhusu sababu za kushindwa kufikia lengo la makusanyo ndani siku 14.

Bashungwa,ametoa wito huo leo Januari 28,2022  jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu mapato na matumizi ya ndani ya halmashauri kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba.

“Wakuu wa Mikoa wahakikishe kuwa halmashauri zote ambazo zimekusanya chini ya asilimia 50 ya lengo la mwaka la makusanyo ya ndani, zinawasilisha maelezo kwa katibu mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, kuhusu sababu za kushindwa kufikia lengo la makusanyo ndani ya siku 14”amesema Bashungwa

Waziri Bashungwa amesema kuwa katika maelezo hayo yabainishe mikakati ya jinsi ya kuboresha mapato ya ndani, katika kipindi cha nusu mwaka kilichosalia (Januari – Juni 2022) ili kuweza kufikia malengo ya makusanyo.

Akitoa taarifa hiyo ya mapato amesema katika kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2021/22 halmashauri ya wilaya ya Hanang, imeongoza kwa kukusanya asilimia 102 ya makisio yake ya mwaka, ikifuatiwa na Halmashauri za Wilaya ya Kaliua, Shinyanga, na Mlele ambazo zimekusanya kwa asilimia 91.

“Aidha,halmashauri za wilaya ya Bumbuli na Kilindi zimekua za mwisho katika kundi hili kwa kukusanya asilimia 27 ya makisio yake ya mwaka, ikifuatiwa na halmashauri ya wilaya ya Bunda ambayo imekusanya kwa asilimia 28 ya makisio yake ya mwaka”ameeleza Bashingwa

Bashungwa amesema katika kipindi hicho halmashauri ya Mji wa Korogwe imekuwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 39 ya makisio yake ya mwaka, ikifuatiwa na halmashauri ya Mji ya Nzega asilimia 42, na halmashauri ya Mji Masasi kwa asilimia 42.

“Katika kundi la halmashauri za Manispaa kwa kipindi cha nusu mwaka kwa mwaka wa fedha 2021/22, halmashauri ya Manispaa ya Kahama, imeongoza kwa kukusanya mapato kwa asilimia 67 ya makisio yake ya mwaka, ikifuatiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Musoma asilimia 65, na Manispaa ya Ilemela asilimia 55.

“Katika kundi hili Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, imekuwa ya mwisho ambapo imekusanya asilimia 37 ya makisio yake ya mwaka ikifuatiwa na Halmashauri za Manispaa ya Kigoma asilimia 38 na Ubungo asilimia 40”alisema

Aidha amesema  halmashauri ya Jiji la Tanga, limeongoza kwa kukusanya mapato kwa asilimia 56 ya makisio yake ya mwaka, ikifuatiwa na Halmashauri ya Jiji la Arusha asilimia 55, na Halmashauri ya Jiji la Mwanza asilimia 54.

Aidha, Halmashauri ya Jiji la Mbeya limekuwa la mwisho, katika kundi hilo ambapo limekusanya asilimia 45 ya makisio yake ya mwaka ikifuatiwa na halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam asilimia 52, na Jiji la Dodoma asilimia 53.

Post a Comment

0 Comments