Iran yakosoa azimio la Baraza Kuu la UN kuhusu Holocaust

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani kitendo cha kutengwa Tehran katika azimio la Holocaust katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kuitaja hatua hiyo kuwa ni utumiaji mbaya wa utawala wa Kizayuni wa Israel wa mifumo na taasisi za kimataifa ili kuficha jinai na uhalifu wake.

Katika taarifa yake iliyotolewa jana Ijumaa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema: “Hatua hiyo ya utawala wa Kizayuni ni jaribio jingine la kutumia vibaya taasisi za Umoja wa Mataifa ili kuficha jinai za kila siku za utawala huo ambazo kwa bahati mbaya zimeambatana na uungaji mkono.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa: "Kama inavyodhihirika kwa kila mtu, jinai za kipindi cha Vita vya Pili vya Dunia zilifanyika kutokana na dhamira mbili za ubaguzi wa kimbari na sera za kujitanua, na hivi sasa utawala wa Kizayuni wa Israel ndio mrithi na mshika bendera wa tabia hizo mbili za kishetani."

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran imesema kuwa: "Mtazamo wa kibaguzi wa utawala huo umefafanuliwa katika nyaraka nyingi za kimataifa, na licha ya msimamo mkali wa jamii ya kimataifa, Israel inasalia kuwa utawala pekee wa kibaguzi wenye itikadi ya kujitanua."

Taarifa hiyo imeongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikilaani mauaji ya halaiki kwa hali yoyote ile, na ndio maana wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, Iran ilikuwa mwenyeji wa wakimbizi wa vita hivyo kutoka katika baadhi ya nchi za Ulaya; wakati huo huo utawala bandia wa Israel umekuwa ukijaribu mara kwa mara kuwatumia wahanga wa Vita vya Pili vya Dunia na Mayahudi kwa ajili ya kuhalalisha vitendo vyake visivyo na haya na vya kichokozi.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa: Utawala huo na viongozi wake umefanya jinai za kila aina hususan jinai dhidi ya binadamu kwa wananchi wa Palestina na raia wa nchi za Magharibi mwa Asia katika kipindi chote cha miongo saba iliyopita. Imesisitiza kuwa, mauaji ya kimbari, mauaji ya kigaidi, maangamizi ya kizazi, kuharibu nyumba na kuwazingira binadamu ni miongoni mwa jinai ambazo utawala wa Kizayuni unaendelea kuzifanya.

Mwishoni mwa taarifa hiyo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza kwamba, kuzuia kutokea tena majanga ya kihistoria kunahitaji utafiti wa kihistoria ambao unapaswa kufanywa bila ya matashi ya kisiasa, na kwa hivyo mienendo hiyo ya kidhalimu haikubaliki, na azimio hilo na Baraza Kuu halitambuliwi kuwa ni makubaliano ya wananchama wote na halikubaliwi.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa siku ya Alhamisi, likiungwa mkono na utawala wa Kizayuni na Ujerumani, lilipitisha azimio la kupiga marufuku ukanushaji wa Holocaust au kinachodaiwa kuwa ni mauaji ya Wayahudi katika Vita vya Pili vya Dunia.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments