Jaji Warioba atoa dira ya Katiba mpya, Tume huru


Unaweza kusema Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba ametoa dira ya kumaliza mchakato wa Katiba mpya baada ya kushauri kupigwa kura za maoni mwaka 2024 wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Kauli ya Jaji Warioba imekuja wakati kukiwa na mvutano miongoni mwa wanasiasa kuhusu mchakato huo, huku baadhi yao wakitaka kwanza yafanyike mabadiliko ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Akizungumza juzi katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Jaji Warioba alisema hakuna sababu ya kuwepo kwa mvutano kwa sababu mchakato wa Katiba hauzuii sheria nyingine kupitishwa.

Jaji Warioba aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoundwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete mwaka 2012, alisema mchakato huo ulikuwa karibu umefikia mwisho, baada ya ukusanyaji wa maoni ya wananchi hadi Katiba Katiba inayoendekezwa na Bunge Maalum la Katiba.

“Baada ya kupitishwa (Katiba inayopendekezwa) ilikuwa iende kwenye kura ya maoni. Lakini Jaji (Damian) Lubuva (aliyekuwa Mweyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi- NEC) akasema kwa sasa tunafanya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu,” alisema.

Jaji Warioba alisema mchakato huo ulipoahirishwa ilitegemewa kwamba baada ya uchaguzi wa mwaka 2015 utaratibu ungefanywa, lakini pia haukufanyika.

Alisema kwa hali ya sasa itakuwa vigumu kukamilisha mchakato huo wa kura ya maoni kutokana na maambukizi ya Uviko-19, kwa kuwa ni lazima ifanyike mikutano ya kampeni, huku pia akigusia hali mbaya ya uchumi.

Huku akishauri viongozi wa vyama vya siasa wakutane kujadili jinsi ya kukamilisha mchakato huo, Jaji Warioba alisema “mimi nimetoa maoni yangu, kwamba nafikiri ingefanywa mwaka 2024 kwa sababu ni mwaka wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Ili kupunguza gharama tuchanganye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kura za maoni.”

Alisema kwa kuwa muda umepita, inabidi ile Katiba Inayopendekezwa itazamwe upya na ifanyiwe maerekebisho.

“Kwa mfano, ukiisoma ile Katiba Inayopendekezwa inasema; “Hii ni Katiba ya Tanzania ya mwaka 2014” haiwezi kuwa Katiba mpaka imeidhinishwa na wananchi,” alidokeza.

Alisema kwa hali ya sasa hakuna haja ya kurudiwa kwa mchakatyo mzima kwani tayari taarifa zote zilishakusanywa.

Tume huru ya uchaguzi

Akizungumzia Tume huru ya uchaguzi, Warioba alisema haina haja ya kusubiri mchakato wa Katiba mpya ukamilike.

“Hakuna ubaya kwenda na yote, mpaka mtakapopata Katiba, lakini mjue Katiba ikipitishwa, haianzi kutumika moja kwa moja. Kwenye Katiba ileile huwa wanatia muda wa mpito ili yarekebishwe mambo fulani fulani,” alisema.

Alisema endapo ushauri wake ukitekelezwa na Katiba ikapatikana mwaka 2024, muda hautatosha kufanya marekebisho na kupata Tume huru ya uchaguzi.

“Ndiyo nasema kwamba, unaweza kufanya mabadiliko ya Tume bila kungojea Katiba mpya, kwa sababu ni sheria ya kawaida.

“Tangu tuwe na mchakato wa Katiba, kuna sheria nyingi tu zimepitishwa na kila sheria inayotungwa msingi wake ni Katiba. Hivi kwa nini ikija kwenye Tume ya katiba mseme ingojee Katiba? Kwa nini hizi nyingine mnatunga bila kungojea Katiba mpya?” alihoji.

Alitoa mfano wa mazungumzo yaliyofanywa mwaka 2014 na viongozi wa vyama vya siasa na rais mstaafu Jakaya Kikwete baada ya kuahirishwa kwa kura za maoni, ambapo walijadili mabadiliko madogo.

“(Mambo) waliyochagua ilikuwa ni Tume ya uchaguzi, uchaguzi wa Rais kwamba apate zaidi ya asilimia 50 ya kura, matokeo ya Rais yahojiwe na mgombea binafsi. Kwa sababu waliamini kwamba kama wangekwenda na referendum (kura ya maoni) wasingekuwa na muda,” alisema.

Akifafanua zaidi, Jaji Warioba alisema katika rasilimu ya Katiba walipendekeza kuwe na sifa zinazojulikana za mtu anayekuwa mjumbe wa Tume huru ya uchaguzi na pia watu wanaotaka kuwa wajumbe wa tume hiyo ni lazima watume maombi ambayo yatachujwa na jopo lililo chini ya jaji mkuu.

“Wakishachuja wanapeleka majina ya kuteuliwa na Rais.”


Mkutano wa vyama

Mkutano wa Baraza la Vyama vya siasa nchini uliofanyika jijini Dodoma Desemba 15 hadi 17, Jaji Warioba alisema ilikuwa ni hatua muhimu ya mazungumzo ya kutafuta maridhiano.

“Jambo la pili, Rais amekubali kufungua mkutano. Lilikuwa ni muhimu kwa sababu ameonyesha utashi wa kisiasa kwamba tunalo tatizo na ni lazima tutafute njia ya kulishughulikia. Hiyo kuja tu kufungua ilikuwa ni muhimu.

“Tatu, aliyoyasema pale, yalikuwa muhimu sana. Alionyesha anajua kuna tatizo na yuko tayari kuliongoza Taifa hili tuweze kumaliza hilo tatizo na alitamka maneno pale kwamba nchi yetu, hakuna aliye na hatimiliki na matatizo tuliyonayo tuyamalize,” alisema.

Warioba alisema hata mazungumzo ya wadau waliohudhuria yalileta matumaini ya kufikia maridhiano.

“Pale yalizungumzwa mambo mengi lakini yaliyojitokeza ni pamoja na mikutano na siasa, tume ya uchaguzi na tatu ni Katiba,” alisema.

Alisema pia Rais alitoa maagizo kwa baadhi ya mambo kufanyiwa kazi likiwemo suala la mikutano ya vyama vya siasa.

Alisema wajumbe wa mkutano huo walitoa hoja zaidi ya hoja 80 ambazo sasa zimeundiwa kikosi kazi kitakachotakata maoni hayo na kuweka maazimio ya kupeleka kwa Rais.

“Matumaini yangu sasa itasaidia, tena siyo kulalamika, kwamba kuna mambo yanayotugawanya, waje na mapendekezo maalumu tufanye nini ili tufikie makubaliano,” alisema.


Mwaka wa maridhiano

Alipoulizwa maoni yake kuhusu mwaka 2022, Jaji Warioba alisema japo mwaka 2021 ulikuwa mgumu kutokana na maambukizi ya Uviko-19 na kifo cha Rais Magufuli, Tanzania ilipita salama.

“Kwa haya yote tuliyopitia, ningeona mwaka 2022 uwe mwaka wa maridhiano, kisha wote kwa pamoja tupambane na matatizo haya kwa pamoja.

“Nchi yetu bado ni ya amani, tusiruhusu tofauti zozote zile zisije zikaingilia umoja wetu. Msingi wetu uwe umoja, mshikamano na amani,” alisema Jaji Warioba.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments