Recent-Post

Kuachiliwa huru wapinzani wa serikali ya Ethiopia; juhudi za kuanzisha mazungumzo ya kitaifa


Baada ya miezi kadhaa ya mzozo na vita nchini Ethiopia, AbiY Ahmed Waziri Mkuu wa nchi hiyo ametangaza msamaha na kuwaachia huru wafungwa mashuhuri wa kisiasa akiwemo kiongozi wa upinzani Jawar Mohammed na maafisa wa chama cha upinzani cha Tigray na hivyo kupiga hatua ya kwanza kwa minajili ya kurejesha utilivu wa kisiasa na kuandaa uwanja kwa ajili ya mazungumzo ya kitaifa.

Tangazo hilo limetolewa baada ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed kutoa taarifa ya mwito wa kutafuta "maridhiano ya kitaifa". Orodha ya wanasiasa waliopewa msamaha ni pamoja na wanachama kadhaa waandamizi wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF), ambao wapiganaji wao wamekuwa kwenye vita na mapigano makali na vikosi vya jeshi la serikali ya Addis Ababa tangu Novemba 2020, pamoja na viongozi mashuhuri wa upinzani kutoka jamii za Oromo na Amhara.

Jawar Mohammed na Eskinder Nega, ambao walikamatwa na kuwekwa kizuizini Julai 2020 kufuatia machafuko makubwa yaliyozuka baada ya kuuawa msanii maarufu wa jamii ya Oromo Hachalu Hundessa, ni miongoni mwa wanasiasa waliopata msamaha huo wa serikali.

Sebhat Nega, Kidusan Nega, Abay Woldu, Abadi Zemu, Mulu Gebregziabher na Kiros Hagos ni miongoni mwa viongozi wa Tigray waliopewa msamaha.

Wizara ya Sheria ya Ethiopia imesema, msamaha kwa Mohammed Jawar na Eskinder Nega umetolewa ili "mazungumzo yajayo ya kitaifa yafanikiwe na yawe jumuishi"

         

Taarifa ya serikali ya Ethiopia imesisitiza kuwa, daima ufunguo wa umoja ni mazungumzo na kwamba, kupatiwa ufumbuzi matatizo ya nchi hiyo ni jambo linalohitajia mazungumzo jumuishi.

Kwa miongo kadhaa sasa Ethiopia imekuwa ikikabiliwa na changamoto muhimu za kiuchumi, kikaumu na kisiasa huku kwa zaidi ya miezi 18 sasa ikiwa imo katika vita na mapigano na wakazi wa maeneo mbalimbali ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika hususan wa jimbo la Tigray.

Japokuwa mivutano na vita baina ya jeshi la serikali kuu na waasi Tigray vimekuwepo kwa muda mrefu, lakini mapigano mapya yaliyozuka kuanzia Novemba mwaka 2020 ni makubwa kuwahi kushuhudiwa katika miaka ya hivi karibuni. Mapigano hayo yalianza baada ya viongozi wa jimbo la Tigray kufanya mambo kinyume na matakwa ya serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed kuhusiana na uchaguzi.  Kwa mntazamo wa serikali ya Addis Ababa ni kuwa, hatua hiyo ilikuwa kinyume cha sheria na ilifanyika katika fremu ya kupigania kujitenga. Ni kwa msingi huo, ndio maana serikali kuu ikaamua kuingia vitani kukabiliana na wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF).

Wapiganaji wa TPLF wa Tigray

 

Vita hivyo viliendelea na katika miezi ya hivi karibuni vilipanua wigo wake katika maeneo mbalimbali ya Ethiopia ukiwemo mji mkuu Addis Ababa. Hadi sasa vita hivyo vimesababisha maafa makubwa kama kupoteza maisha maelfu ya raia huku ripoti za asasi za kimataifa zikionyesha kuharibiwa pakubwa kambi za wakimbizi, kufanyika uporaji, kushuhudiwa vitendo vya kuwabaka na kuwanajisi wanawake na mauaji ya umati.

Kushadidi mapigano nchini Ethiopia kumewalazimisha maelfu ya raia wa Ethiopia kukimbilia katika mataifa jirani kama Sudan. Hivi karibuni Umoja wa Mataifa ulitangaza kuwa, mzingiro wa misaada ya kibinadamu unaukwaza umoja huo katika kuwafikia raia milioni 5 wanaohitajia misaada ya kibinadamu katika jimbo la Tigray.

Martin Griffiths, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kibinadamu anasema kuwa: Mgogoro wa jimbo la Tigray nchini Ethiopia unahesabiwa kuwa doa jeusi kwa dhamira za walimwengu.

Kushadidi vita nchini Ethiopia na kupanuka wigo wake kumefungua mlango wa kuongezeka uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo ambapo mbali na madola ya Ulaya na Marekani kuondoa raia wake katika nchi hiyo mataifa hayo yametoa indharia kuhusiana na mustakabali wa nchi hiyo. Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, kuzidi kuwa mbaya hali ya mambo nchini Ethiopia kumeufanya Umoja wa Afrika kuzungumzia hatari ya kugawanyika nchi hiyo.

Kifaru cha jeshi la Ethiopia kikiwa vitani

 

Hayo na mengineyo ndio yaliyomsukuma Waziri Mkuu Abiy Ahmed aje na mpango wa mazungumzo na maridhiano ya kitaifa, mpango ambao umepokewa kwa mikono miwili na wapiganaji wa TPLF wa Tigray ambao kwa kurejea nyuma na kuondoka katika majimbo ya Amhara na Afar kimsingi wametangaza utayari wao wa kufanya mazungumzo ya amani na serikali ya Addis Ababa. Uamuzi huo ulifuatiwa pia na tangazo la serikali ya Ethiopia la kuhitimisha operesheni za kijeshi dhidi ya waasi.

Filihali hatua ya Abiy Ahmed ya kutangaza kuwaachilia huru wafungwa wa kisiasa akiwemo kiongozi wa upinzani inalenga kuboresha hali ya kisiasa ya nchi hiyo. Demeke Mekonnen, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ethiopia anasema kuwa: Ajenda za mazungumzo ya kitaifa zitajadiliwa muda si mrefu na kwamba, kuna uwezekano wa kufikiwa ufumbuzi wa kudumu wa mzozo wa ndani wa nchi hiyo.

Moja ya mambo ambayo yanayotarajiwa kujadiliwa katika mazungumzo hayo ni kipengee nambari 39 cha katiba ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa kipengee hicho, kila umma, kaumu na raia ana haki isiyo na masharti ya kujiainisha hatima na mustakabali wake ikiwemo haki ya kujitenga.

Alaa kulli haal, inaonekana kuwa, Waziri Mkuu Abiy Ahmed kwa mara nyingine tena amefanikiwa kudhibiti hali ya mambo na kama mazungumzo ya kitaifa nchini Ethiopia yataanza, basi kuna uwezekano wa kuboreka mazingira ya kisiasa ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Post a Comment

0 Comments