Recent-Post

MABINTI WANAFUNZI TAASISI YA USTAWI WA JAMII WAJENGEWA UWEZO


Watoa Mada na baadhi ya wanafunzi walioshiriki kongamano la kumjengea binti uwezo katika picha ya pamoja mwishoni mwa juma mara baada ya kufanyika kongamano hilo katika ukumbi wa maktaba wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii Kijitonyama Jijini Dar es Salaam 

Mhadhiri Msaidizi idara ya Ustawi wa Jamii Taaluma ya Taasisi ya Ustawi wa Jamii Bi.Rufina Khumbe akifungua kongamano la kumjengea binti uwezo kwa niaba ya Mkuu wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii Dkt Joyce Nyoni lililofanyika katika ukumbi wa maktaba wa Taasisi hiyo mwishoni mwa juma hili Jijini Dar es Salaam. 

Mwalimu wa shule ya Msingi Kijitonyama Mwl.Sophia Mbeyela akitoa wasilisho katika kongamano la kumjengea binti wa kike uwezo lililofanyika mwishoni mwa juma katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii Jijini Dar es Salaam.

OWESOME YOUTH VISION GROUP chama cha wanafunzi wa Kike wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii kijitonyama, Taasisi iliyo chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum leo wamefanya Kongamano la mabinti Kumjengea mtoto wa kike.

Kongamano hilo lilifunguliwa na Mhadhiri Msaidizi Kutoka idara ya Ustawi wa Jamii taaluma Rufina khumbe kwa niaba ya mkuu wa Taasisi Dkt.Joyce. Nyoni.

Akiongea wakati wa kufungua kongamano hilo Bi Rufina alisema thamani ya mwanamke ni asili kupitia maandiko ambapo Mungu alibaini uhitaji wa Mwanamke na ndipo akamtengeneza mwanamke kukamilisha uumbaji, kibali na baraka za Mwanaume na jamii zipo kwa mwanamke hivyo binti ni dhahabu, binti ni lulu. Thamani yake ni kubwa sana katika dunia hii, anapaswa kujitambua, kujithamini na kuachilia zile baraka ambazo mungu amempatia kwa kufanya yaliyo mema na kukubalika na jamii yake.

Lengo kuu la kongamano hilo ni Kumnyanyua binti; kwa kumpa elimu na kumjengea uwezo wa kujitambua na kuwa na ujasiri wa kuthubutu na kutumia fursa zilizopo ikiwa ni pamoja na Elimu , uongozi, kupaza sauti kwa niaba ya mabinti wenzie, kujiamini na kujisimamia pamoja na ujasirimali.

Sambamba na hilo pia wanafunzi wa kike wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii walipatiwa elimu kuhusiana na nidhamu, elimu na maisha ya chuo kwa kipindi ambacho wapo Taasisi na namna sahihi ya kuweka malengo, nidhamu na namna ya kukabiliana na changamoto za mazingira, na kuweza kufikia malengo alisema Mhadhiri Rufina.

Mada mbali mbali ziliwasilishwa na wachangia mada waalikwa ambapo "Elimu juu ya haki na usawa wa kijinsia" iliwasilishwa na mwalimu Sophia Mbeyela kutoka Shule ya Msingi Kijitonyama.

Vile vile mada kutoka kwa mkurugenzi wa Amani Project ambayo inahusisha watu wenye uhitaji maalum. Elimu ya Afya na maadili ambayo iliwasilishwa vyema na ndugu Asumpta Godfrey ambaye ni mwanzilishi wa Be Hamble project na mtangazaji wa redio.

Sambamba na hayo elimu juu ya binti kutambua fursa na kuzitumia hasa anapokuwa chuo na namna sahihi ya kujiwekea malengo na kuhakikisha kufikia malengo ambapo ilitolewa vyema na ndugu Asma Jamida kutoka wasafi media. Kwa upande wake Shamira Mshangama kutoka Wasafi Tv alizungumzia uongozi na mwanamke namna ambavyo binti anaejitambua, kujithamini na kujiwekea malengo anaweza na kuwa kiongozi bora kutoka ngazi ya Taasisi hadi Taifa Nini afanye na nini kuepuka, mbinu na taratibu za kufanya; changamoto na namna yakukabiliana nazo.

Taasisi ya Ustawi wa Jamii inatambua nafasi kubwa iliyonayo ya kutoa elimu bora ya kitaaluma kwa wanafunzi inayowaandaa kuhudumia jamii lakin pia Kutoa elimu kwa Jamii inayozunguka Taasisi na Jamii ya watanzania kwa ujumla ili kupunguza matatizo ya Kijamii ya mtu mmoja mmoja, familia, na Makundi maalum kama ambavyo Mh. Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzainia Samia Suluhu aliona upekee katika ustawi wa jamii na kuunda Wizara mpya ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ambayo Taasisi ya Ustawi wa Jamii iko chini yake.

Taasisi ya Ustawi wa Jamii itaendelea kumuunga mkono Mh. Rais Samia kwa kutoa elimu kwa jamii kupitia Vyombo vya habari, vyumba vya mihadhara ya kitaaluma na Kituo chake cha Elimu, Ushauri na Msaada wa kisaikolojia pamoja na mikutano na wanajamii ili kupunguza vitendo viovu na vya ukatili kwa Watoto, wanawake na makundi maalum vinavyoendelea kushamiri hapa nchini.

Post a Comment

0 Comments