Recent-Post

Maiti za wanawake watatu zaokotwa kando ya mto


Wanawake watatu wanaokadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 18 hadi 30 wameuawa na watu wasiojulikana na miili yao kukutwa pembezoni mwa mto eneo la Nyakato/Buzuruga jijini Mwanza.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Gidion Msuya ameliambia Mwananchi kwa simu leo Jumatano Januari 19, 2022 kuwa uchunguzi unaendelea kuhusu tukio hilo ikiwamo kuwambua marehemu na kuwasaka waliohusika na mauaji hayo.

Miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya kanda Bugando kwa ajili ya utambuzi na uchunguzi zaidi,” amesema Kaimu kamanda Msuya.

Ingawa hadi Saa 12 jioni hii haijajulikana ni lini, wapi na kwa njia gani mauaji hayo yalifanyika, lakini miili ya wanawake hao ilionyesha kuwa walikatwa na kitu chenye ncha kali kutokana na majeraha yaliyoonekana maeneo ya shingoni.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa mtaa wa Mecco eneo la Nyakato zilikookotwa maiti hizo, Scolastica Barnabas amesema pamoja na kukutwa na majeraha shingoni, miili yao ilikuwa tupu haijavikwa nguo.

Tunaviomba vyombo vya dola vifanye uchunguzi wa kina kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria wote waliohusika kufanya mauaji haya,” amesema Scolastica.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, Gpdfrida Yohana na Jonas Mghira waliozungumza kwa nyakati tofauti waliiomba jamii kusaidia kutoa taarifa zitakazowezesha wahusika wa mauaji hayo kubainika na kufikishwa mahakamani na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria.

Post a Comment

0 Comments