"Nchi za Magharibi zilizofaidika na utumwa ziwape fidia Waafrika"

 

Nchi za Magharibi zilizohusika na kustafidi na biashara haramu ya utumwa zimetakiwa kuzilipa fidia nchi za Afrika kutokana na jinai za utumwa na ukoloni.

Mwito huo umetolewa na wataalamu wanaofuatilia taathira za utumwa wa Afrika Kusini na kuongeza kuwa, nchi za Magharibi zinapaswa pia kuwaomba radhi wananchi wa nchi za Afrika kwa madhila na udhalilishaji waliofanyiwa katika enzi za utumwa.

Mustafa Mheta, mtafiti na Mkuu wa Dawati la Afrika la taasisi ya wanafikra ya Media Review Network yenye makao yake jijini Johannesburg amesema, "Afrika haiwezi kufikia maridhiano na Magharibi katika suala la utumwa, hadi pale Waafrika watakapoombwa radhi na nchi za Magharibi zilizonunua watumwa (wa Kiafrika), na kulilipa fidia bara la Afrika."

Biashara ya haramu ya utumwa

Ameeleza bayana katika mahojiano na shirika la habari la Anadolu kuwa, kinachosikitisha zaidi ni kuwa, mataifa yaliyofanya biashara ya utumwa, yangali yanastafidi na utumwa huo hadi leo hii. 

Naye Saber Ahmed Jazbhay, mwanaharakati maarufu wa kisheria na kisiasa wa Afrika Kusini ameashiria suala la kulipwa fidia nchi za Afrika kutokana na dhulma, mateso na unyanyasaji uliofanywa na Wamagharibi zama na utumwa na kusema: Maridhiano hayawezi kupatikana bila ya uadilifu wa kiuchumi.

Kwa mujibu wa takwimu rasmi, watu zaidi ya milioni 40 kote duniani ni wahanga wa utumwa mamboleo, huku wanawake na wasichana miongoni mwao wakitumika kama watumwa wa ngono.

Post a Comment

0 Comments