Recent-Post

Nigeria: Magenge ya wabeba silaha yatangazwa kuwa ni makundi ya ugaidi

 

Kabla ya tangazo hilo, magenge hayo yamekuwa yakitambuliwa kama makundi ya majambazi.

Hatua hiyo inajiri mwezi mmoja baada ya mahakama kuu mjini Abuja kutoa uamuzi kama huo kuhusu magenge hayo.

Magenge hayo ya uhalifu yanayodhibiti sehemu kubwa nchini Nigeria, yamekuwa yakiwateka nyara wanafunzi wa shule, kuwapiga na kuwateka nyara watu, kuwabaka na kuwalazimisha baadhi ya wahanga kuwa watumwa wa ngono.

Kwa mujibu wa sheria, hatua ya kuyatambua magenge hayo kuwa ni magaidi inatoa mamlaka kwa jeshi la Nigeria kupambana nayo.

Majimbo ya kaskazini magharibi na sehemu za kati kaskazini, yameathiriwa kwa muda mrefu na magenge hayo yanayotekeleza mashambulizi kila mara.

Genge la wabeba silaha jimboni Zamfara

 

Magenge yenye silaha nzito nzito yamekuwa yakipora mifugo, kuwateka nyara watu na baadaye kudai kikomboleo ili kuwaachilia huru.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Nigeria inakabiliwa na ukosefu mkubwa wa usalama hasa katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ambapo makundi kadhaa likiwemo la Boko Haram yamehatarisha usalama wa raia katika maeneo hayo.

Tokea mwaka 2009 hadi sasa, Nigeria imo vitani kupambana na magaidi wa Boko Haram ambao wametangaza utiifu wao kwa genge la kigaidi la Daesh. 

Hujuma na mashambulio ya  Boko Haram yameshaua watu wasiopungua 36,000 na kusababisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi ndani na nje ya Nigeria hasa katika maeneo yanayopakana na Ziwa Chad.

Post a Comment

0 Comments