Rais Samia Aipongeza Wizara Ya Utamaduni, Sanaa Na Michezo Kwa Mikakati Na Ubunifu Mkubwa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan ameipongeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa ubunifu na mikakati kabambe ya kuandaa matamasha mbalimbali ya sekta hizo yanayoleta tija kwa wananchi na kuielekeza kukaa pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii ili kuja na mkakati wa kuandaa matamasha bora zaidi ili yatumike kuitangaza Tanzania na kutoa ajira kwa wananchi.


Rais Samia ameyasema haya leo Januari 22, 2022 kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi wakati akizindua Tamasha la Utamaduni la Mkoa wa Kilimanjaro lililoratibiwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Chama cha Umoja wa Machifu Tanzania kupitia Mwenyekiti wa Machifu Mkoa wa Kilimanjaro, Frank Mareale na Mkoa wa Kilimanjaro.

Mhe. Rais amesema, kutokana na umuhimu mkubwa wa Utamaduni aliamua kuunda wizara maalum ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ili kutunza maadili, kuzalisha ajira na kukuza michezo na kuwachagua viongozi vijana kuongoza wizara hiyo ambapo amesisitiza kuwa wanaisimamia kwa ubunifu mkubwa.

Ameongeza kuwa katika kipindi kifupi Wizara imeweza kufanya mapinduzi makubwa kwenye sekta hizo na kutaka kuendelea kushirikiana na wadau ili kuboresha zaidi.

Ameyataja baadhi ya matamasha ya kihistoria ya utamaduni ambayo yameratibiwa na Wizara kwa ubunifu wa hali ya juu katika kipindi hiki baada ya Serikali yake kuingia madarakani kuwa ni pamoja na Tamasha la Utamaduni la Bagamoyo, Tanga, Tamasha la Machifu la Utamaduni la Mwanza na Morogoro.

Aidha, ameipongeza Wizara kwa kuandaa Mkutano wa machifu uliowakutanisha machifu wote jijini Dodoma na kuazimia kuwa na jukwaa la pamoja ambapo amefafanua kuwa yeye atakuwa Mwenyekiti wa jukwaa hilo.

Amesisitiza kuwa Serikali yake itaendelea kuimarisha bajeti ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ili kuendelea kubaini, kulinda na kuendeleza utamaduni wa watanzania kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.

Naye Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Pauline Gekul amesema Sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo ni sekta mtambuka za nguvu ya kimkakati kwa taifa na zinatoa fursa ya ajira kwa vijana wengi.

Amemhakikishia Mhe. Rais kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano, ubunifu na weledi ili kuhakikisha malengo ya Serikali na Ilani ya Chama cha Mapinduzi yanatekelezwa kikamilifu.

 John Mapepele-WUSM
TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments