Recent-Post

Sababu daraja la nne kufunika kidato cha nne

     


Matokeo ya mitihani ya kidato cha nne 2021 yanaonyesha kundi la wanaopata daraja la nne linaendelea kukua ikilinganishwa na miaka miwili iliyopita, huku wadau wa elimu nchini wakionyesha wasiwasi kwa baadhi ya wahitimu hao huenda wakashindwa kuendelea na ngazi mbalimbali za elimu kutokana na kukosa vigezo.

Akitangaza matokeo ya mtihani huo jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Godfrey Msonde, alisema kati ya watahiniwa 422, 388, waliopata daraja la nne walikuwa 248, 966 sawa na asilimia 51.46.

Hii ni sawa na kusema kuwa zaidi kidogo ya nusu ya wahitimu wa kidato cha nne mwaka 2021, walipata daraja hilo, hivyo kujiweka katika hatihati ya kutoendelea na masomo hasa kidato cha tano hapo baadaye.

Soma zaidi: Matokeo kidato cha nne haya hapa

Kwa kuwa si wote watakaopata fursa ya kuendelea na kidato cha tano kwenye shule za binafsi, wadau wameshauri vyuo vya ufundi kuongezewa uwezo ili viweze kuwachukua kwa wingi.

Akizungumza na Mwananchi jana, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Ezekiah Oluoch, alisema dawa ya wahitimu wanaopata daraja la nne ni kwenda vyuo vya ufundi.

‘‘Hawa waende kozi za kujiajiri. Ni muhimu vyuo vya ufundi na kati viwe vingi, maana ili nchi yetu iweze kuendelea tunahitaji asilimia 65 ya Watanzania wawe na ujuzi katika fani mbalimbali, ‘‘alisema.

Akiamini katika mtazamo na kauli alizotoa baada ya matokeo ya mwaka jana,Oluoch aliendelea kusema:

“Kwa hiyo Profesa Adolf Mkenda (Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia), analazimika kuwekeza zaidi katika vyuo vya kati na ufundi ili kupokea theluthi mbili ya watahiniwa wanaokosa nafasi ya kuendelea kidato cha tano. Huko wanaweza kufanya vizuri.”


Mwenendo wa daraja la nne kwenye matokeo

Takwimu za miaka mitatu kuhusu mwenendo wa wahitimu wanaopata daraja la nne zinaonyesha mwaka 2019 daraja la nne walikuwa asilimia 48.6 ya watahiniwa 422,722, mwaka 2020 wakiwa asilimia 50.74 ya watahiniwa 434, 654.

Mwaka jana iliongezeka zaidi hadi asilimia 51.5 ya watahiniwa 483, 820. Hata hivyo mwaka 2015 ulikuwa na hali mbaya zaidi, asilimia 67.91 ya 240,996 waklipata daraja hilo.

Hii inamaanisha kuwa watahiniwa watano kati ya kumi wamepata daraja la nne matokeo ya mwaka 2021, ikilinganishwa na wastani wa watahiniwa sita kati ya kumi wa mwaka 2015.

Akizungumza baada ya matokeo ya mwaka jana, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Faraja Kristomus , alieleza kuwa hali hiyo inaleta taswira kuwa kuna changamoto kwenye mfumo wa ufundishaji.

Dk Faraja ambaye baada ya kutafutwa tena jana, alisisitiza kuwa na mtazamo wa kile alichokieleza mwaka jana, alisema licha ya mfumo wa kufundishia kubadilishwa kutoka kwenye kukariri hadi umahiri, walimu wengi waliopo pembezoni mwa nchi hawajapata mafunzo ya kutosha kuhusu mfumo huo hali inayowasababishia kuendelea kufundisha kizamani.

“Katika shule nyingi za pembezoni walimu hawana mafunzo ya mfumo huu wa kumjenga mwanafunzi kwenye umahiri, shule pia hazina mazingira wezeshi yanayomfanya mtoto atumie umahiri wake katika kujifunza na kwa bahati mbaya mitihani ikija inakuwa imetungwa kwa mfumo huo,” alisema Faraja.

Kwa upande wake, Oluoch mwaka jana alisema hali hiyo inachangiwa na ongezeko la wanafunzi shuleni ambayo haiendani na ongezeko la walimu.

Oluoch alisema shule nyingi zipo katika mazingira magumu ya kufundishia na kujifunza hali inayoendelea kukuza namba ya wanafunzi wanaopata daraja la nne.

“Shule zaidi ya 4,000 zipo vijijini na kwenye ngazi ya kata ambako mazingira ya kufundishia ni magumu, walimu wachache na hawapati motisha, vitabu havipatikani kulingana na uwiano wa wanafunzi, hata watoto kukaa muda mrefu bila kupata chakula inawapotezea morali ya kuzingatia kinachofundishwa.

“Katika hili, Serikali ikubali wazazi wachangie chakula shuleni ili watoto hata wakimaliza vipindi ile saa nane wabaki kujisomea hadi jioni. Hii itawasaidia hata wale ambao wakirudi nyumbani hawapati nafasi ya kusoma kutokana na mazingira,” alisema Oluoch.


Mwenendo wa daraja sifuri

Kwa mujibu wa Necta, mwenendo wa sifuri unaonyesha 2012 zilikuwa asilimia 56.92 ya watahiniwa 458,139, mwaka 2013 asilimia 42.91 ya watahiniwa 404,083.

Mwaka 2014 asilimia 30.24 ya wanafunzi 297,488, mwaka 2015 asilimia 32.09 ya watahiniwa 443, 633 na mwaka 2016, asilimia 29.65 ya 408,372.

Mwaka 2017 sifuri zilikuwa asilimia 22.43 ya watahiniwa 385, 767,mwaka 2018 zilikuwa asilimia 20.73 ya 426,988.

Mwaka 2019 zilikuwa asilimia 19.4 ya 422,722, mwaka 2020 zilikuwa asilimia 13.96 ya 434,654 na mwaka 2021 sifuri zilikuwa asilimia 12.7 ya watahiniwa 483,820.

Post a Comment

0 Comments