Recent-Post

Serikali yasema kuna idadi kubwa ya wazee, watoto mitaani

 Serikali imesema idadi ya wazee na watoto walioko mitaani bado ni tatizo ambalo bila kuwa na usimamizi linaleta picha tofauti.

 Kauli hiyo imetolewa leo Januari 25, 2022 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima wakati akizungumza na watoto wa kituo cha kulelea watoto na wazee cha Upendo Hombolo jijini Dodoma.

Amesema ukatili unaofanywa na wazazi na baadhi ya watu wanaoishi na Makundi hayo imekuwa chanzo watu wengi kuzikimbia familia zao kwenda mtaani.

Dk Gwajima amesema ukatili umekuwa mkubwa katika familia ambazo nyingi hazijali hata wanapoona watoto wanaondoka nyumbani au wazee na kwenda kuishi maisha ya tabu.

"Asilimia 70 ya ukatili huo wanafanyiwa watoto wa kike kwa hiyo roho mbaya ya ukatili imeelemea upande mmoja wa watoto wa kike, hatari sana hii," amesema Gwajima.

Waziri ameomba viongozi wa dini kushirikiana na Serikali katika kumaliza changamoto hizo kwani wakiamua kwa pamoja wanaweza kukomesha vitendo hivyo

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Amon Mpanju amesema sheria ya kulinda watoto na makundi mengine zipo isipokuwa utekelezaji wake ndiyo unakuwa tatizo.

Mpanju amesema Wizara hiyo mpya itakuwa na jukumu la kuhakikisha watoto na wazee wanakuwa salama wakati wote kwa kuihusisha jamii katika ulinzi na usimamizi wake.

Amesema kwa sasa Serikali inaendelea kutoa elimu kuhusu madhara ya ukatili na kuomba jamii ione mzigo wa kusaidia kutunza familia ambazo hazijiwezi.

Akisoma risala kwa niaba ya Sista Mkuu wa kituo hicho, Sista Radiance amesema wanakabiliwa na changamoto ya bili kubwa ya madeni ya umeme na gharama za matibabu.

Sista Radiance amesema tangu kituo hicho kilipojengwa 1978 na kuzinduliwa na Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1983 wamehudumia idadi kubwa ya watu wakiwepo watoto wa kuanzia siku moja na wazee wasiojiweza na huduma zao ni bure.

 

Post a Comment

0 Comments