Recent-Post

Shahidi kesi kina Sabaya adai kulazimishwa kukiri makosa

Mshitakiwa wa tano katika kesi ya uhujumu uchumi, Sylvester Nyegu (26), amedai kuwa akiwa katika Gereza Kuu la Kisongo, Arusha, Ofisa wa Takukuru, Ramadhan Juma alimlazimisha kukiri makosa na kumuahidi kumtoa na kumfanya kuwa shahidi.

Aidha ameieleza mahakama kuwa hakuwahi kupokea mgao kutoka kwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya wa Sh2.4 milioni kama ilivyodaiwa mahakamani hapo na shahidi wa 13 wa Jamhuri, Ramadhan Juma.

Nyegu ni miongoni mwa washitakiwa saba wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, akiwemo aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya.

Nyegu alitoa madai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, akiongozwa na Wakili anayemtetea Sylvester Kahunduka, wakati alipoanza kujitetea mahakamani hapo baada ya kukutwa na kesi ya kujibu mwishoni mwa wiki.

Shahidi huyo ambaye ameieleza mahakama yeye ni mfungwa namba 614/2021, akiwa gerezani Julai 18 mwaka jana, walifika watu waliokuwa wanajitambulisha ni maofisa kutoka Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) waliokwenda kuwahoji watuhumiwa wote saba.

Alidai kuwa, Juma aliyekuwa shahidi wa 13 wa Jamhuri katika kesi hiyo alimlazimisha kukiri makosa.

“Nakumbuka nikiwa gerezani Kisongo walikuja watu waliojitambulisha ni maofisa wa Takukuru na kusema wanakuja kutuhoji kuhusu hizi tuhuma ambapo mmoja wao, alijitambulisha kwa jina la Juma.

“Wakati ananihoji alikuwa ananilazimisha nikiri haya mashtaka haya yanayonikabili na kwa ahadi atanitoa na nitakuwa shahidi wake, lakini nilikataa nikamwambia siwezi kukiri kitu ambacho sijakifanya na sikijui,” alisema.

Alikanusha kutenda kosa la utakatishaji fedha la kupokea Sh90 milioni iliyoandikwa kwenye hati ya mashtaka.

Post a Comment

0 Comments