Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Kiuchumi na Kijamii, ECOSOC, Collen Vixen Kelapile ameiteua nchi ya Tanzania kuwa Mwenyekiti Mwenza wa Jukwaa la Saba la Wadau Mbalimbali wa Masuala ya Sayansi, Teknolojia na Uvumbuzi katika kutekeleza Agenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, SDGs.
Rais wa ECOSOC pia amemteua Balozi Profesa Kennedy Gastorn ambaye ni Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, na Balozi Sergiy Kyslytsya, Mwakilishi wa Kudumu wa Ukraine katika Umoja wa Mataifa kuwa wenyeviti wa Jukwaa hilo.
Akizungumza na waandishi habari wa Umoja wa Mataifa baada ya uteuzi huo, Balozi Gastorn amesema ni heshima kubwa sana kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuweza kupata nafasi hii kuwa Mwenyekiti Mwenza wa Jukwaa hili.
Ameongeza kuwa, “pamoja na mambo mengine hii ni ishara ya jinsi ambavyo Tanzania na diplomasia yake inazidi kukubalika katika macho ya kimataifa chini ya uongozi wa mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania."
Amesema Tanzania kama mwanachama mwingine katika Umoja wa Mataifa, itaitumia nafasi hiyo kubadilishana uzoefu na kuonesha mipango yake, mafanikio na changamoto katika sekta hiyo na kuweza kukuza uhusiano na kubadilishana uzoefu na wadau wengine kimataifa.
Halikadhalika Balozi Gastorn amebaini kuwa, kama Mwenyekiti mweza, Tanzania itatumia nafasi hiyo kuwaunganisha wadau wa masuala ya sayansi, teknolojia na uvumbuzi katika kutekeleza ajenda ya maendeleo endelevu ya mwaka 2030 ya Umoja wa Mataifa.
Akifafanua madhumuni ya jukwaa hilo la wadau wa masuala ya Sayansi, Teknolojia na Uvumbuzi, Balozi Gastorn amesema, “madhumuni ya jukwaa hili ni kuwakutanisha wadau mbalimbali wa masuala ya sayansi, teknolojia na uvumbuzi ili kujadili na kubadilishana uzoefu kwa namna masuala hayo yanavyoweza kurahisisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, SDGs ya mwaka 2030.”
0 Comments