Serikali ya muda ya Mali imependekeza kwa majirani zake wa Afrika Magharibi kwamba kipindi cha mpito cha kurejesha demokrasia baada ya mapinduzi ya kijeshi ya 2020 kirefushwe kwa miaka mitano.
Awali, serikali ya mpito ilikubali kufanya uchaguzi wa rais na wa bunge Februari mwaka huu wa 2022, miezi 18 baada ya Kanali Assimi Goita kuongoza mapinduzi ya kijeshi yaliyoiondoa madarakani serikali ya Rais Boubacar Ibrahim Keita.
Mkutano uliokuwa umepewa jukumu la kutoa mapendekezo juu ya ratiba ya uchaguzi ulisema Alkhamisi iliyopita kwamba uchaguzi mkuu unapaswa kucheleweshwa kwa kati ya miezi sita na miaka mitano.
Baada ya mkutano wake na Rais wa Ghana, Nana Akufo-Addo ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) yenye wanachama 15, Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali, Abdoulaye Diop amesema amependekeza kiwango cha juu zaidi cha muda huo.
Msemaji wa ECOWAS hajatoa taarifa yoyote kuhusiana na suala hilo.
Jumuiya hiyo inajitahidi kushikilia msimamo wake dhidi ya mapinduzi ya kijeshi nchini Mali katika eneo hilo la Magharibi mwa Afrika ambalo katika miaka ya karibuni lilionekana kupoteza sifa yake ya kuwa "ukanda wa mapinduzi" barani Afrika.
Kanali Assimi Goita alifanya mapinduzi ya pili Mei 2021 alipomuondoa madarakani rais wa mpito ambaye alichukua hatamu baada ya kupinduliwa Keita na kuchukua wadhifa huo yeye mwenyewe.
0 Comments