Vinasaba vya askari wa Afrika Kusini wanaolinda amani DRC vyakusanywa ili kubaini baba za watoto

Jeshi la Afrika Kusini limepeleka timu yake kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo MONUSCO, ili kuchunguza vinasaba (DNA) vya watoto na wanawake waliobakwa na walinda amani ili hatimaye kuthibitisha iwapo watuhumiwa ni walinda amani kutoka Afrika Kusini na kisha watoto hao watambue baba zao na pia kupatiwa malezi.

Sakata la ukatili wa kingono unaofanywa na walinda amani wa Umoja wa Mataifa kule wanakohudumu, limesababisha Afrika Kusini ambayo nayo ina walinda amani wake nchini Kongo DR ichukue hatua kuhakikisha siyo tu kitendo hicho kinatokomezwa bali pia watoto wanatambua baba zao ili waweze kuhudumiwa.

 Kanali Anina Els, Mkuu wa kitengo cha sheria katika jeshi la Afrika Kusini, SANDF, anasema, “hivi sasa timu yetu iko hapa kwenye ujumbe wa MONUSCO, kusimamia ukusanyaji wa sampuli za DNA za akina mama na watoto kwa ajili ya kutambua baba halisi wa mtoto na madai ya matunzo ya mtoto.”  

Mkurugenzi wa Uamuzi wa Kitabibu kutoka jeshi la Afrika Kusini, Brigedia Jenerali D. Tempelhoff amesema wameanza kazi hiyo tangu mwaka 2017 kukusanya sampuli za vinasaba kutoka kwa kila mwanaume mlinda amani anayekwenda kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa.

Tempelhoff ameongezea kwa kufafanua: "Hii inafanyika kabla hawajaenda, na hii inatuwezesha kushughulikia madai yoyote kutoka kwa mama mwenye mtoto nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ya kwamba kuna baba wa Afrika Kusini, hivyo tunaweza kumpata haraka mtuhumiwa au kuthibitisha kuwa askari wetu hana kosa.” 

Yewande Owadia ambaye ni Mkuu wa Nidhamu MONUSCO anasema hatua hiyo inaimarisha uwajibikaji. 

“Hii ni njia ambayo wadai na wale wanaohusika kwenye mchakato wanaona kabisa kwamba nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zimejizatiti kushughulikia madai ya malezi kutoka kwa baba na pia kutokomeza ukatili wa kingono”, ameeleza afisa huyo wa MONUSCO.

 Umoja wa Mataifa unatumai kuwa mchakato huo utaleta suluhu kwa manusura wa ukatili wa kingono na watoto wao. 

Jeshi la Afrika Kusini lina walinda amani wake kwenye kikosi cha kujibu mashambulizi, FIB cha MONUSCO kinachohudumu mashariki mwa Kongo DR.../

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments