Wachimbaji wadogo Chunya walia gharama kubwa matibabu ya magonjwa ya zinaa

Wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika kijiji cha Itumbi kilichopo wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, wamelalamikia gharama kubwa za matibabu ya magonjwa ya zinaa katika zahanati na vituo vya afya wanavyokwenda kupata huduma.

Wachimbaji hao wameeleza hayo leo Ijumaa Januari 14, 2022 mbele ya Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMRI), Profesa Yunus Mgaya ambaye amefanya ziara katika machimbo hayo na kusikiliza kero zao.

Mchimbaji mdogo, Issa Mohamed amesema kuna changamoto ya maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi ambayo yanachochewa na mwingiliano wa watu kutoka mikoa mbalimbali nchini na kukosekana kwa dawa za kufubaza makali ya ugonjwa huo.

“Kwa kweli hali ni mbaya sana katika maeneo ya machimbo, hata upatikanaji wa huduma za afya ni shida. Zahanati na vituo vya afya vipo mbali, hivyo inasababisha wagonjwa kukata tamaa na kusababisha kupoteza maisha kutokana na kukosa matibabu hususan dawa za ARVs,” amesema.

Ameiomba Serikali kuwafikia na kuweka kambi kwa ajili ya kupima maambukizi na kutoa dawa kwa watakaokutwa na virusi sambamba na tiba ya magonjwa ya zinaa ambayo wamekuwa wakitozwa fedha nyingi za matibabu.

“Inafika wakati wagonjwa kukata tamaa kutokana na kutembea umbali mrefu kufuata huduma na wanapofika wanadaiwa fedha nyingi kwa ajili ya kupatiwa matibabu. Naiomba Serikali itutazame kwa jicho la huruma watu wa maeneo ya machimbo,” amesema mchimbaji huyo.

Kwa upande wake, Profesa Mgaya amesema NIMR imeweka utaratibu wa Kliniki inayotembea ili kuwafikia wagonjwa na kufanya vipimo vya magonjwa ya kifua kikuu, Ukimwi, magonjwa ya zinaa, saratani ya shingo ya kizazi na kuhamasisha chanjo dhidi ya maambukizi ya Uviko-19.

“Gari letu lipo kwenye zahanati ya kijiji cha Itumbi, linaendelea kutoa huduma na kuna wataalam licha ya kuwepo kwa uhaba ambao unachangia kushindwa kuwafikia maeneo mbalimbali. Hivyo, tutahakikisha mnafikiwa kupatiwa huduma na vipimo ili kulinda afya zenu na kupata kinga na madawa ya kufubaza VVU,” amesema.

Mganga Mkuu wa Hosptali ya Wilaya ya Chunya, Daison Andrew amesema watahakikisha ndani ya mwezi mmoja wanapelekwa wataalam wa afya kwa ajili ya kutoa elimu ya upimaji magonjwa ya kuambukizwa na kuwapatia dawa za ARVs kwa watu watakaokutwa na maambukizi.

“Kimsingi tunawapongeza kwa kuwa wawazi kwani dawa za ARVs zinatolewa bure katika vituo vyote vya afya na zahanati, lakini kuhusu matibabu ya magonjwa ya zinaa ni lazima kuchangia na nitalifuatilia hilo kama gharama ziko juu kwa watoa huduma,” amesema.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments