WANANCHI WENYE MGOGORO WA ENEO MDA MREFU LOLIONDO WAKUTANA BAADA YA KAULI YA MKUU WA MKOA WA ARUSHA

KAULI ya hivi karibuni ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella kuhusiana na eneo lenye mgogoro wa muda mrefu la km za mraba 1500,  lililolopo, Loliondo, wilayani Ngorongoro Mkoani Arusha, imezua taharuki kubwa kwa wananchi wa eneo hilo na kusababisha kukutana na kutoa tamko la kupinga kauli hizo.


Kauli hiyo ya Mongela iliyotaja eneo hilo la km 1500 na kuwa atasimamia maslahi mapana ya Taifa na ya Mkoa wa Arusha, aliitoa tarehe 11.1.2022, alipokuwa katika ziara ya siku 5 ya kikazi katika wilaya ya Ngorongoro.

Wakizungumza na waandishi wa habari, wakiwa na mabango yenye jumbe mbalimbali ya kupinga kauli hizo, katika Mkutano wa hadhara uliofanyika  katika uwanja wa kijiji cha Olorieni, Tarafa ya Loliondo, walisema kauli hizo zimewapa mashaka na kushindwa kuelewa hatma yao na hivyo kupitia chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Ngorongoro, wameomba kukutana na Rais Samia ambaye wana imani naye.

Akitoa tamko kwa niaba ya wananchi, mbele ya viongozi wa mila (malaigwanani), madiwani, viongozi wa CCM wilaya ya Ngorongoro, Diwani wa Kata ya Alash,  Mathew Siloma alisema Mkuu wa Mkoa kwa kujua au kutojua ameuanzisha upya, mgogoro uliopo, wakati ilishapita mamlaka yake ya kiutawala.

“Mwaka 2016, Waziri Mkuu Kasim, Majaliwa aliunda tume ya kukusanya na kuwasilisha kwake mapendekezo ya namna ya kumaliza mgogoro huo”alisema.

Siloma alisema badae tume iliwasilisha taarifa kwa Waziri Mkuu April 2017.Hata hivyo waziri Mkuu alisema Serikali itafanyia kazi mapendekezo ya tume ikiwemo suala la usimamizi na utumiaji wa pamoja wa eneo la mgogoro.Mpaka sasa Serikali haijaweza kurasimisha mapendekezo au kuweka hadharani.

Alisema kitendo cha Mkuu wa Mkoa kuanzisha upya mgogoro kwa kutembelea eneo hilo na kusema linatengwa, inakiuka misingi ya utawala bora, kuingilia mahakama na kuzua taharuki kubwa kwa wananchi wa Tarafa za Sale na Loliondo.

Siloma alisema madiwani kutoka Kata zinazoathirika, Viongozi  wa vijiji, Viongozi wa mila na wanawake waliiomba Serikali kuchua hatua zifuatazo.

Kutambua km za mraba 1500 kuwa ni ardhi ya vijiji na sio eneo la Hifadhi, kuachana kabisa na azma ya kutenga eneo la vijiji kwajili ya uwindaji kwani wananchi wa Loliondo hawana ardhi ya ziada ya kuhamia, kuweka wazi taarifa za kamati ya Gambo iliyowasilishwa kwa Waziri Mkuu April 2017.

Pia Kuheshimu kesi iliyopo mahakamani na kuacha kuwasumbua Wananchi wakati kesi ikindelea kadri ya zuio lililotolewa Agost 2018 na kuomba kumuona Rais Samia ili kumueleza uhalisia wa mgogoro huo wa kutungwa na wahifadhi kwa kuwalinda wawekezaji bila kutambua maslahi ya maisha ya wananchi.

Kiongozi wa mila (laigwanani) Rafaeli Long’oi alimwomba Rais Samia Suluhu kuangalia Wanangorongoro kwa jicho la pili kwani tangu Mwaka 1959 waliondolewa Serengeti na kupelekwa Loliondo na kujengewa miundombinu kama shule, majosho na mengineyo, lakini leo wanaambiwa waondoke.

Diwani viti maalum tarafa ya sale Kijoolu Kakeya, kwa niaba ya wanawake alisema kuwa wanawake wa wilaya hiyo wanapata shida hivyo kuomba wamwone Rais Samia awawapiganie wanawake wenzake kwani wao ndo wanaoteseka kutokana kubeba mzigo mkubwa katika familia.

 Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Ngorongoro, Ndirango Ole Senge alisema kama chama wamepokea malalamiko ya wasiwasi na watayafikisha kunakohusika yashughulikiwe kwa haki na kupata muafaka.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella alipokuwa ziarani wilayani Ngorongoro alisema Serikali imesikia mengi kuhusiana na eneo lenye mgogoro lakini Serikali haitaonea mtu yoyote, awe mwekezaji au Mwananchi ila kama kuna maslahi mapana ya Taifa yatazingatiwa hayo.
Wananchi jamii ya kifugaji wakiwa wamebeba mabango kupinga eneo lao km 1500 kumegwa
Diwani wa kata ya Alash Mathew  Siloma akitoa tamko kwa niabaya ya wananchi ya kupinga eneo lao la ardhi kumegwa

Diwani viti maalum kutoka tarafa ya Sale Kijoolu Kakeya  akiongea kwa niaba ya wanawake alimuomba Rais Samia Suluhu kuingilia kati sakata hilo
Kiongozi wa kimila Laigwanani Rafael Long'oi alimuomba Rais kuangalia mgogoro huo kwa jicho la pili

Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi wilaya ya Ngorongoro Ndirago Ole Senge akiongea na wananchi hao
                                             
                                      Na Pamela Mollel,Ngorongoro

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments