Wanaojenga mradi wa maji wa bilioni 1.9 Handeni walia ‘mauzauza’


Eneo la bwawa la Kwenkambala lililopo kata ya Kwediyamba wilayani Handeni mkoani Tanga ambalo ujenzi wake unadaiwa unasuasua kutokana na imani za kishirikina. Picha na Rajabu Athumani.
Mradi wa kuchimba bwawa la maji Kwenkambala wilayani Handeni mkoani Tanga unao gharimu Sh1.99 bilioni umekwama kuendelea kwa madai kuwa ni kutokana na imani za kishirikina kwenye eneo hilo kwa vifaa kuharibika mara kwa mara.

Hayo yamebainishwa na msimamizi wa mradi huo kutoka kampuni ya Civil Loths Construction LTD, Kulwa Juma katika ziara ya kamati ya siasa Mkoa wa Tanga ya kukagua miradi ya maendeleo wilayani Handeni, akisema changamoto waliyonayo ni vifaa kuharibika mara kwa mara.

Juma ametaja changamoto nyingine kuwa ni watumishi wa kampuni hiyo kuripoti kuwa kuna mambo ya ajabu yanaoneka kwenye mradi.

Amesema wapo madereva wanadai kuona vitu vya ajabu ikiwamo nyoka mkubwa anayefuata nyumba greda wakati wakifanya kazi.

"Huu mradi unasuasua kwasababu ya kuharibika vifaa vyetu vya kufanyiakazi mara kwa mara, tukiwa kazini vinaharibika hata ukitengeneza baadae tatizo linarudi tena, tuombe Ruwasa walipe fidia kwa hawa wananchi wanaodai Sh15 milioni maana ndio sababu ya haya mambo yanayotokea", amesema mhandisi Kulwa.

Amesema wamekuwa wakipeleka vifaa vizima yakiwemo magreda kwenye eneo la ujenzi lakini vifaa hivyo vikianza kufanya kazi vinaharibika baada ya muda mfupi.

Juma amedai kuwa wakati wakiendelea na mradi huo baadhi ya wananchi wamekuwa wakilalamika na kutishia kuwa mradi huo hautakamilika kutokana na kutolipwa fidia.

Mkuu wa Wilaya ya Handeni (DC), Siriel Mchembe kwenye ziara hiyo amewalaumu Ruwasa kushindwa kuwalipa fedha wananchi wanaodai fidia na kuagiza uongozi wa Ruwasa ngazi zote kuhakikisha wananchi husika wanalipwa fedha zao haraka ili mrafi kuendelea.

Amesema kuwa Ruwasa haiwatendei haki wazee kwa kushindwa kuwalipa fidia.

“Hivi kweli Ruwasa Sh15 milioni tunajadili mpaka leo, na mbauya zaidi sasa wazee wale kila siku wanaahidiwa na wanatafuta maeneo mengine ya kulima sasa hawana maeneo na hawana fedha” amesema na kuongeza

Kwa hiyo wale wakandarasi hapa wakaanza kupata hofu, inawezekana ni maruweruwe au ni hofu, mi sijayaona wao ndio waliyoyaona kwa hiyo mi sitaki kuyasemea lakini ninachotaka kusema badala ya kuanza kuwalaumu wazee kuwa kuna maruweruwe tuanze kwanza, wazee wamekosewa na wameonewa na Ruwasa” amesema DC huyo

"Mradi huo utawanufaisha wananchi kutoka katika kata sita sawa na watu 28,735 ambapo mradi unatakiwa kukabidhiwa Februari 16 mwaka huu kwa maelezo ya mkataba ila mpaka sasa hakuna dalili za kukamilika" amesema Mchembe

Baada ya maelezo hayo mjumbe wa kamati ya siasa Mkoa wa Tanga, Mohamed Ratco akatoa maagizo ya kushughulikiwa changamoto zote za eneo hilo haraka kwani Serikali haiamini mambo hayo.

Amemuagiza mkuu wa wilaya ya Handeni Siriel Mchembe kuhakikisha wanaodai wanalipwa kwani sio jambo jema Serikali kutoa fedha nyingi kusaidia wananchi hao 28,735 lakini mradi unasuasua kwa sababu ambazo sio za msingi.

Meneja Ruwasa wilaya ya Handeni, Hosea Mwingizi amekiri kuwepo kwa tatizo la kasi ndogo ya utendaji kazi kwenye bwawa hilo ambalo lina ukubwa wa ujazo wa mita 2,222,817 wakati majitaji ya wanufaika ni mita za ujazo 2,095,650 kwa mwaka.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments