Wastaafu wanapolazimika kujihakiki mara mbilimbili

Ule mwezi wa ‘Njaanuary’ ambapo mzee wetu mstaafu na miaka yake 79 analazimika kufika makao makuu ya wilaya au mkoa aliopo kwenye majengo ya kibubu kinachomuwekea akiba yake ya uzeeni ili kuhakikiwa kama bado yupo na anapumua hewa ya bure ya Mungu isiyokuwa na tozo, ili aendelee kupokea pensheni, umefika tena.

Naam, wakati wengine wanahangaika na ada, kodi na madeni mengine ya Njaanuary, mstaafu yeye anatakiwa kujihakiki ili aendelee kupokea pensheni yake ya ‘laki si pesa’ aliyoiweka mwenyewe.

Hajajua kwa nini vibubu vinavyomtunzia akiba yake vinaweka masharti na kanuni kibao zinazoishia kumkwaza yeye mwenye chake, utafikiri chao!

Ndiyo, mwezi huu mzee wetu mstaafu na miaka yake 79 analazimika kutoka huko Mahezanguu au Kibugumo alikojichimbia baada ya kustaafu, apande mabasi hadi makao makuu ya wilaya au mkoa ili aendelee kupokea ‘laki si pesa’ yake. Mwenyewe alikatwa kwenye mshahara wake ili imsaidie kwenye uzee wake!

Hebu tukumbushane kidogo hapa wapenzi wasomaji. Si kila mstaafu ambaye mara tu baada ya kustaafu aliamua kubanana hapa hapa mjini. Kuna wengine wengi tu waliamua kurudi kijijini kwenye makaburi ya baba na mama zao Magoroto na Mwamamilato, mbali kabisa na majengo ya kibubu kinachomtunzia akiba yake ya uzeeni.

Kumtaka mstaafu kufika makao makuu ya wilaya au ya mkoa ya kibubu chake kila ‘Njaanuary’ kuhakikiwa kama bado yupo ili aendelee kupokea akiba aliyojiwekea mwenyewe ni mateso.

Yaa, ni mateso. Yaani mzee wetu huyu badala ya tumuache amalizie maisha yake hapa duniani kwa amani tunaanza kumsumbua tena ili tu kuweza kupokea alichotunza mwenyewe kwa mshahara wake. Ni mateso kwamba atoke Madongokuinama alipo, alipe nauli ya kwenda na kurudi, na mjini hana ndugu wa kufikia kwa hiyo inamlazimu alale ‘lojingi’ kwa gharama zake ambazo hatarejeshewa! Ni mateso.

Na hapo hatujasema kama mstaafu wetu katika shida zake alirogwa akachukua ule mkopo wenu wa siku hizi ambao benki zetu hazitofautishi riba na tozo ya kumshika mstaafu asiyekuwa na kipato chochote na riba na tozo za mfanyabiashara na kumfanya apokee Shilingi elfu arobaini na sita (Sh46,000) tu kwa mwezi kwa miaka mitatu inayofuata ya kulipa mkopo wake! Halafu hizi hizi azipange kwenda mkoani makao makuu ya kibubu chake kuhakikiwa kila Njaanuary! Ni maumivu plus! Mbona mnamtafuta mstaafu wetu maneno kwa kosa lisilokuwa lake?

Kwamba mstaafu anaweza kuelekea Kinondoni katikati hapo na mkewe na vitegemezi vyake wakaendelea kuvuta pensheni yake ya ‘laki si pesa’! Sasa? Si zake? Kwani anamuibia mtu? Si alikatwa mwenyewe kwenye mshahara wake? Mbona wanaomtunzia chake cha uzeeni alichokatwa mwenyewe kwenye mshahara wanamuwekea masharti magumu kuliko yeye mwenye akiba yake? Ndio tekelinalotujia? Mbona enzi za Marhum NPF hayakuwepo haya? Watu walikuwa wanahakikiwa mara moja tu katika ustaafu wao na kiiila kitu kinakuwa bien!

Kwa hakika, mstaafu angependa inapotokea yeye kumrudia Muumba wake, mkewe na vitegemezi wake waendelee kupokea pensheni yake hadi yule wa mwisho kati ya wale wanne aliotakiwa kuwaandikisha enzi za ajira afikishe miaka 18 ndio ataona akiba yake aliyojiwekea itakuwa imekwenda kihalali! Lakini haya mambo ya mtu hakuchangia chochote lakini ndio anaweka masharti kibao katika kinachoaminika ni kulinda akiba ya mstaafu? Hapana! Wanaoiba ni wengine!

Mstaafu anaomba kuharakisha kusema kuwa hapingi watunza kibubu cha akiba yake ya uzeeni kuchukua tahadhari za kuzuia wizi kwenye kibubu chake. La hasha! Anachosema ni kwamba kama kuna wezi wa akiba ya uzeeni ni huko huko jikoni. Watazamane na kuchunguzana.

Mstaafu wetu angetaka katika nyakati hizi za teknolojia kubwa na iliyotukuka, watunza kibubu chake cha ustaafu watafute namna nyingine na si hii ya kuwaongezea wastaafu maumivu yao ya kumhakiki kama yupo hai na anastahili kupokea ‘laki si pesa’ yake ya mwezi au la, isiwe hii ya kumfanya atoke Mahezangulu alikojichimbia kwa nauli ya kwenda na kulala mjini na kurudi shamba aliko.

Pensheni yenyewe ya kugharamia hivyo kila ‘Njaanuary’ inapofika iko wapi? Hii hii ambayo imeshafanyizwa na tozo na riba ya mkopo wa benki usiotofautisha mstaafu na mfanyabiashara?

Mstaafu wetu angependa kuvisifu hivi vibubu vya akiba yake ya uzee ambavyo ukipiga simu na kuwaambia kwamba wewe ni mstaafu na huwezi kutembea kwenda kuhakikiwa wanakufuata mara moja na kufanya uhakiki wa hapohapo nyumbani kwako.

Kwa hili nawapa pongezi. Kwa mjini. Sijui kama huduma hii itapatikana ukiwa kijijini Magoroto au Kibugumo!

Tatizo si mke au vitegemezi vya mstaafu kuendelea kupokea pensheni ya baba yao wakati mwenyewe ameishatangulia Kinondoni katikati ya mwaka. Wanachukua chao tu baba yao alichokitolea jasho. Tatizo limo humohumo kwenye vibubu wakati mzee mstaafu ameishatangulia Kinondoni mwaka uliopita lakini bado 10 wengine kama yeye wanaendelea kuvuta pensheni yake, kama vile bado yupo hai!

Wakati bado wastaafu wakiendelea kusubiri ubunifu wa mtu kuanzisha Wizara mpya ya ‘Wizara ya Nanii na Nahii na Wastaafu’, bado ‘Njaanuary’ ni ngumu mno hadi Mstaafu anajua kwa nini binadamu wanaweza kula embe na maganda yake lakini hawawezi kufanya hivyo kwa papai wakati yote ni Matunda! Tusomane hapa Ijumaa Ijayo.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments