Watano wajeruhiwa ajali ya basi Tabora

  Watu watano wamejeruhiwa baada ya basi lililokuwa na zaidi ya abiria arobaini kupinduka katika eneo la Cheyo Manispaa ya Tabora.

Basi hilo la Abood ambalo linafanya safari za Tabora-Dar es salaam limepata ajali leo Jumapili Januari 9, 2022 muda mfupi baada ya kutoka mjini Tabora.

Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Dk Yahaya Nawanda ameeleza kuwa abiria watano waliopata majeraha wamepelekwa kupata matibabu katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora, Kitete.

Amesema abiria wengine ambao hawakupata majeraha, wameendelea na safari kwa kutumia basi la kampuni ya Kisbo.

"Utaratibu umefanywa abiria kuendelea na safari na waliojeruhiwa kupelekwa Kitete kwa matibabu"

Shuhuda wa ajali hiyo, Sadick Yassin mkazi wa Cheyo amesema aliona basi hilo likipita pembeni ya barabara sehemu ambayo mabasi hayapiti na kupinduka.

Dereva alipita pembeni ya barabara jirani na reli na kushindwa kulimudu ambapo lilipinduka" amesema.

Mmoja wa Polisi aliyeomba hifadhi ya jina lake kwa vile sio msemaji, amesema chanzo ni uzembe wa dereva wa basi kupita sehemu isiyo rasmi kwa mabasi.

Dereva wa basi hilo ambaye jina lake bado halijafahamika amedaiwa kukimbia baada ya ajali kutokea.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments