Mashambulizi hayo yamejiri wiki moja baada ya zaidi ya watu wengine 200 kuuawa katika hujuma ya majambazi katika jimbo la Zamfara, kaskazini magahribi mwa Nigeria.
Taarifa zinasema watu 18 wameuawa katika shambulizi dhidi ya jamii ya Ncha, katika sehemu ya Bassa, jimbo la Plateau, huku watu wengine 34 wakiuawa katika sehemu za Nakuna na Wurukuchi, jimbo la Niger.
Tukio katika jimbo la Niger limeonekana kuwa la kulipiza kisasi, baada ya kutokea mauaji wiki chache zilizopita pale wapiganaji wa kijamii katika eneo hilo kuua watu kadhaa waliokuwa wamejihami kwa silaha na waliokuwa wanashutumiwa kwa kuwahangaisha raia.
Wiki iliyopita Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari aliahidi kuwa serikali haitalegea katika vita vyake dhidi ya majambazi wanaowahangaisha wananchi.
Akizungumza baada ya mauaji ya Zamfara, alisema mashambulizi hayo dhidi ya watu wasio na hatia ni kitendo cha kusikitisha sana. Alisema serikali yake inafungamana na ahadi ya kukabiliana na ugaidi na hivyo aliwahakikishia wananchi walio katika maeneo yaliyokithiri vitendo vya uhalifu kuwa serikali ina azma ya kuwaangamiza wahalifu wote.
Maeneo ya kaskazini na kaskazini mashariki mwa Nigeria yamekuwa yakishuhudia ongezeko kubwa la vitendo vya uhalifu huku serikali ikiwa mbioni kurejesha amani bila mafanikio. Mwaka jana majambazi waliwateka mamia ya watoto wa shule na kudai vikomboleo kabla ya kuwaachilia huru. Idadi kubwa ya wanafunzi bado wako mikononi mwa watekaji nyara.
Wiki iliyopita Jeshi la Nigeria lilitangaza kuwa tokea mwezi Mei mwaka jana, limewaua majambazi 537 na kuwakamata wengine 374 huku raia 452 waliokuwa wametekwa nyara wakiachiliwa huru.
0 Comments