Wimbi la wizi wa mifugo limerejea kwa kasi mkoani hapa baada ya kuwepo utulivu wa zaidi ya miaka 17.
Kitovu cha wizi kimetajwa kuwa ni Kijiji cha Mbabala ambacho kipo kilomita 20 kutoka Dodoma mjini.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Onesmo Lyanga amesema ni suala la muda tu, lakini hakuna mtu atakayesalia mbele ya kikosi chake imara kilichojipanga kikamilifu kukabiliana na uhalifu huo.
Kwa kipindi cha miezi sita, jumla ya ng’ombe 84 na nguruwe 36 wanatajwa kuibwa, hiyo ni kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa juzi kwenye mkutano uliohusisha vijiji vya Mbabala, Bihawana, Mpalanga, Nholi, Mwitikila, Mhangwe na Ibugule.
Miaka ya nyuma mkoa ulikuwa unaongoza kwa wizi wa mifugo, lakini operesheni iliyofanywa mwaka 2002 hadi 2004 na aliyekuwa kamanda wa polisi wa mkoani hapa, Wolfugang Gumbo ilisaidia kuweka hali ya utulivu.
Hivi sasa Wilaya ya Bahi inatajwa kuongoza kwa wizi wa mifugo, lakini tayari viongozi wamekitaja Kijiji cha Mbabala kuwa kituo cha kupokea na kuchinja mifugo ya wizi ambayo hubebwa usiku kupelekwa mabucha ya mjini.
Mkutano wa viongozi
Viongozi wa vijiji vya Mbabala, Bihawana, Mpalanga, Nholi, Mwitikila, Mhangwe, Ibugule na vilivyopo jirani walifanya mkutano wa siku mbili wakitafakari njia wanazoweza kutumia ili kudhibiti wizi huo.
Diwani wa Mbabala, Paskazia Mayala alikiri kuwepo tatizo hilo katika kata yake, akisema wanaofanya kazi hiyo wanafahamika lakini cha ajabu wamekuwa na tabia ya kutishia watu ili wasiwasumbue.
Mayala alisema hata nyumba zinazofanya biashara hiyo zinajulikana, watu wanaosafirisha wanajulikana lakini wanakijiji wanaogopa kuwakamata sababu wanaonekana kuwa na mtandao mrefu hadi kwa baadhi ya polisi.
“Ng’ombe wanaibwa usiku, wanaletwa hapa, wanachinjwa na kuchunwa ngozi kisha wanapelekwa kwenye mabucha huko mjini, lakini cha ajabu ni kwa nini nyama zinapitishwa huko na polisi wapo lakini hawafanyi kitu, matokeo yake sisi tunaanza kutishiwa,” alisema Mayala.
Diwani wa Ibugule, Blandina Magawa alisema hali siyo nzuri katika kata yake na kata jirani, kwa kuwa wizi wa mifugo, ikiwamo ng’ombe na nguruwe umekuwa ni mkubwa, lakini wanaoibiwa ni ng’ombe wa kulima ambao ni tegemeo.
Magawa aliwataja aliowaita ‘magalagaja’ wa mifugo kwamba wamekuwa na tabia ya kwenda kwenye maboma ya wafugaji na kutaka kununua mifugo, lakini huchunguza na kuwasiliana na wenzao, wanakuja kuiba nyakati za usiku wa manane kisha ng’ombe wanachinjwa na haraka wanaondoka.
Katibu wa Kikundi cha Sungusungu Tarafa ya Mwitikila, Didas Ngogomba alisema hali si nzuri kwa wafugaji na maisha yao yamekuwa ya hofu wakati wote, licha ya kujitahidi kuwa walinzi wa mifugo yao.
Ngogomba alisema wanafanya kila juhudi na mbinu za kukabiliana na watu hao, lakini bado wanashindwa na kila mara taarifa zinakuja kuwa mifugo imechukuliwa, lakini wanapofuata nyayo huishia katika Kijiji cha Mbabala na wapo baadhi ya watu wanaojigamba kuwa hawatawaweza.
0 Comments