Mvua yaharibu ekari 100 za mazao Tanganyika


Zaidi ya ekari 100 za mazao zimeharibiwa wilayani Tanganyika baada ya mvua ya mawe iliyoambatana na upepo mkali kunyesha.

Akizungumza na Mwananchi leo Januari 26,2022  mkulima wa tumbaku kijiji cha Igalula, John Shija amesema mvua hiyo ilinyesha Januari 24, 2022 na kuleta athari hizo.

“Yalianza mawe kidogo baadaye yakaongezeka yakajaa, ukitoka nje unakanyaga juu ya mawe nikachungulia tumbaku yangu nikaona matawi yanashuka chini,”amesema Shija

“Ilipokata nikatoka kuangalia shamba langu la tumbaku lenye ukubwa wa ekari mbili na nusu limeisha, mahindi ekari tatu na maharage nusu ekari yameharibika,”

Ofisa ugani wa kata ya Mpandandogo, Edwin Makoye amesema katika kata hiyo mazao ya wakulima zaidi ya 34 yameathiriwa na mvua hiyo.

“Mazao yariyoharibiwa ni mchanganyiko tuna tumbaku ekari 64, mahindi ekari 42, maharage ekari 3, mhogo ekari 5 na karanga ekari 1,” amesema

Ofisa kilimo mazao wilaya ya Tanganyika, Sephania Waya amesema zao lililoathirika zaidi ni tumbaku na kwamba mazao yanayokomaa kwa muda mfupi hakuna uwezekano wa kuyaokoa.

“Tunaendelea kufanya tathimini ili kujua ukubwa wa tatizo, niombe wakulima kupitia hii athari tujifunze tukate bima ya mazao, kwasababu tungekuwa na uhakika wa kulipwa,”amesema Waya.

Mkuu wa wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu aliyefika eneo hilo ameiagiza ofisi ya Mkurugenzi kuwapatia mbolea wakulima wa tumbaku.

“Niwaombe Mkurugenzi, Bodi ya Tumbaku na wanunuzi na nyie AMCOS mkae mjadiliane namna gani mtakavyoratibu kuongeza mbolea kwa wakulima,”

“Kupitia michango ya wadau ikiwamo ofisi yangu, itumike kununua mbolea kwaajili ya tumbaku, kwa mazao mengine wakulima walime alizeti,” amesema Buswelu

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments