Asilimia 60 ya vijana walipima VVU 2020


Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) imesema asilimia 60 ya kundi balehe la vijana wa kati ya miaka 15-24 walipima na kujua hali zao kwa mwaka 2020.

Hata hivyo, katika matokeo hayo kundi la wasichana balehe na wanawake vijana lilikuwa mara mbili au tatu ya vijana wenzao wa kiume kwenye maambukizi.

Hayo yamesemwa leo Februari 3, 2020 na Ofisa Ufuatiliaji na Tathmini Tacaids, Laiser Nyangusi wakati wa mkutano wa waandishi wa habari kuhusu hali ya maambukizi kwa kundi la vijana nchini.

“Takwimu hizo zinaonyesha bado kundi la asilimia 40 halijajua hali zao, lakini imeonyesha maambukizi hayo yanaenea kwa kasi zaidi kwa kundi la wasichana balehe umri wa miaka 15-24 kwa asilimia 2.1 ikiwa ni mara tatu zaidi ya vijana wa kiume kwa asilimia 0.6,” amesema Nyangusi.

Amesema kati ya wenye VVU wapya 77,000 waliokutwa na maambukizi mapya mwaka 2019, asilimia 28 walikuwa miaka 15 mpaka 24 na kati ya hao asilimia 67 walikuwa wasichana balehe na wanawake vijana huku wavulana wakiwa asilimia 23.

Amesema wasichana wengi wanaathirika kutokana na ndoa za kulazimishwa ambazo zinawaweka hatarini kupata mimba zisizotarajiwa, utoaji mimba na maambukizi ya magonjwa na zinaa na VVU.

“Wasichana wanaathirika zaidi kutokana na mila na desturi, mimba za utotoni, ngono za mapema, maambukizi ya magonjwa ya ngono, kutokuwa na maamuzi, unyanyasaji wa kijinsia na mengineyo,” amesema Nyangusi.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments