Recent-Post

Askofu Niwemugizi aomba msamaha wa madeni hospitali ya Ngara na Biharamulo


Askofu wa Jimbo la Rulenge-Ngara, Severine Niwemugizi amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan atoe agizo kwa mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) itoe msamaha wa zaidi ya Sh326 milioni inazodai katika hospitali teule za Wilaya ya Ngara na Biharamulo mkoani Kagera.

Ametoa ombi hilo leo, Jumanne Februari 22, 2022 katika sherehe za Jubilee ya miaka 25 ya Askofu Severine Niwemugizi ambapo amesema hospitali ya Ngara inadaiwa na TRA zaidi ya Sh213 milioni huku hospitali ya Wilaya ya Biharamulo ikidaiwa na mamlaka hiyo zaidi ya Sh113 milioni.

"Hospitali hizi mbili teule (Ngara na Biharamulo) zinahudumia watu maskini wengine wanashindwa kumudu gharama za matibabu, kwa hakika zikifungwa hospitali hizi wananchi wataumia, tunaomba madeni tuliyonayo ya TRA tusamehewe," amesema Askofu Niwemugizi

Soma zaidi:Niwemugizi:Rais Samia usikubali kulinganishwa na Mungu

Pia amemuomba Rais Samia asaidie hospitali hizo kupata vibali vya ajira ili ziweze kuajiri watumishi watakaosaidia kuboresha huduma katika hospitali hizo.

"Tunaomba tusaidie kupata vibali vya ajira ili kuboresha huduma, tutoe huduma bora kwa wananchi," amesema Askofu Niwemugizi

Wakati huo, Askofu Niwemugizi amemuomba Rais Samia kusaidia eneo la kanisa la Jimbo la Rulenge-Ngara lililotwaliwa na halmashauri ya wilaya Ngara lirejeshwe chini ya umiliki wa kanisa hilo.

"Eneo la ardhi lilipojengwa kanisa kuu la jimbo, sehemu yake ilichukuliwa na kujengwa kambi ya wakimbizi kwa maafikiano kwamba wakiondoka eneo litarudi kwa kanisa, lakini walipoondoka kanisa lilipotaka kulirejesha halmashauri ikalichukua," amesema

Ameongeza; "Pia eneo la Kanisa kuu, upande wa pili lilipoanza kujengwa barabara nalo tulinyang'anywa isivyo haki, naomba turudishiwe eneo hilo," ameomba Askofu Niwemugizi

Post a Comment

0 Comments