Bobali aibukia ACT Wazalendo

Aliyekuwa Mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali amejiunga na Chama cha ACT Wazalendo baada ya kuwa kwenye mgogoro na chama chake.

Bobali ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa CUF (Juvicuf), amejiunga na chama hicho wakati kikianzisha kampeni ya "Shusha Tanga, Pandisha Tanga" awamu ya pili.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Februari 5 jijini Dar es Salaam, Bobali amesema amevutiwa na sera za ACT Wazalendo lakini pia amechoshwa na migogoro ndani ya Cuf.

"Sera na ajenda za ACT Wazalendo ndiyo kivutio kikubwa kilichonileta hapa, najisikia niko nyumbani kwa sababu watu niliowakuta wote ninawafahamu.

"CUF imejifia kifo cha kawaida, nilivumilia nikijua kuna mwisho lakini wapi. Dhamira iliyopo ndani ya Cuf sio kupigania wananchi, ni kusubiri Cuf ife watu wagawane mali za chama," amesema Bobali.

Awali akimkaribisha Bobali, katibu mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu amesema chama hicho kimeanzisha awamu ya pili ya operesheni ya Shusha Tanga, Pandisha Tanga iliyoasisiwa na Maalim Seif Sharif Hamad Machi 18, 2019.

Amesema kupitia operesheni hiyo, wanatarajia kuvuna wanachama wengi kutoka vyama vingine na wake wasiokuwa na vyama.

"Tumekuwa tukipata maombi kutoka kwa watu mbalimbali kwenye vyama vingine, tukaona tuanzishe operesheni hii ili kuwapokea hawa na wengine wanaotaka kujiunga na chama chetu," amesema Shaibu.

Wakati Bobali akipokelewa ACT Wazalendo, chama cha Cuf nacho leo kimewapokea wanachama 33 kutoka ACT Wazalendo.

Post a Comment

0 Comments