DK TULIA:BUNGE LIMEKOSA MUNKARI SI HOJA

         

Spika wa Bunge la 12, Dk Tulia Ackson amesema suala la kurusha vikao vya Bunge mubashara (Bunge Live) ni suala ambalo linazungumzika na mwananchi anaweza kutoa malalamiko kwa Spika kama ataona hakutendea haki na kauli ya mbunge aliyoitoa bungeni.

Mkutano huo ulifanyika Jumatatu ya wiki hii kwenye ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa jijini Dodoma na ulifanyika kwa mtindo wa waandishi wa habari kuuliza maswali kwa Spika naye kuyajibu.

Dk Tulia alifanya mkutano huo wa kwanza tangu achaguliwe kushika wadhifa wa Spika Februari Mosi, mwaka huu akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Job Ndugai aliyejiuzulu Januri 6, mwaka huu.

Swali. Je, utarudisha matangazo mubashara ya vikao vya Bunge

Jibu: Hili ni jambo linalozungumzika kwa kuangalia sababu zilizofanya wakati ule lisiwepo na sasa liwepo na tutazungumza na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (Nape Nnauye), halafu tuone namna ya kulifanyia kazi.

Lakini na ninyi waandishi wa habari, tutahitaji mawazo yenu kwa sababu wakati mwingine Bunge kuwa ‘Live’ ni hoja nzuri ukiitazama tu hivi juu, lakini lazima utazame pia ni kitu gani kinaenda ‘Live’ kwa hao wananchi.

Nafikiri ni mambo tunayoweza kushauriana kwa maana sisi Bunge, upande wa Serikali lakini na nyinyi wahusika. Kwa sababu hata nyinyi waandishi wa habari si kila kitu ukienda mahali utataka kuandika kama habari.

Swali: Je, mwananchi asiye mbunge, anaweza kuleta malalamiko bungeni kama ataona kuna jambo fulani pengine hajatendewa haki namna lilivyosemwa bungeni.

Jibu: Hili jambo liko kikanuni, kama kuna mwananchi anayeona amekosewa kwa maelezo yalitolewa bungeni anaruhusiwa kuja na kanuni zimeweka wazi utaratibu.

Anaandika barua kwa Spika kwamba mchango wa mbunge fulani, si lazima ajue tarehe kwa sababu sisi tuna taarifa zote. Yeye akishajua ni mbunge gani anaandika yale malalamiko na sisi tunayafanyia kazi kama yalivyowahi kufanyiwa kazi huko nyuma.

Hata wabunge wenyewe wakituhumiana mle ndani huwa tunachukua hatua, mwingine anaweza kuwa amesemewa jambo ambalo ni la uongo mle ndani, au mwingine anaweza kuwa amefanya jambo la uongo lakini kuhusu Serikali. Hizo kanuni zipo na zinaendelea kufanya kazi.

Yakijitokeza mazingira kama hayo bila shaka tutafuata utaratibu ambao tumejiwekea kwa maana kama mtu anayo malalamiko yeye ayalete tu sisi tutayafanyia kazi na yeye atapata fursa ya kusikilizwa na pia atamsikiliza huyo ambaye atakuwa anatuhumiwa halafu maamuzi yatachukuliwa.

Swali:Mbunge anapofungiwa kuhudhuria vikao vya Bunge nani anaumia, kati yake na anayehitaji uwakilishi bungeni?

Jibu: Wabunge kwa idadi yetu tupo 393, sasa ule siyo mkutano wa hadhara ni mkutano maalumu kwa ajili ya shughuli maalumu kwa hiyo lazima kuwe na namna maalumu ya kuendesha ule mkutano, ukishaufanya kwamba ule mkutano kila mtu atafanya jambo lake analolitaka kidogo inakuwa ngumu na ndio hata hapa mmoja ameuliza hata mtu wa nje akisemwa vibaya anaruhusiwa kuja. Kanuni zinaruhusu kutokana na mazingira ya jambo lenyewe.

Mtu anayeumia ni kweli mwananchi anayehitaji uwakilishi. Huyu mwakilishi wake kwa kuzikosea kanuni hawezi kuendelea kukaa mle ndani kwa sababu tu wananchi wanaumia.

Kuumia kwa wananchi ni kwamba yeye pengine hayupo, lakini kama nilivyosema Bunge lina wabunge 393 na katika Bunge moja siyo wabunge wote watapata nafasi ya kuuliza maswali, siyo wabunge wote watapata nafasi ya uwakilishi.

Je, wale wananchi kule wanakuwa na hali gani. Serikali inaendelea na shughuli zake ilizozipanga kwenye eneo la huyu mbunge haliachi kupeleka maendeleo kwa sababu mbunge wake yuko nje.

Maumivu ni yale ya kawaida tu, hata mimi nisingetamani kusikia mbunge wangu yuko nje ya Bunge, ningetamani kumwambia fuata ule utaratibu usije ukatolewa maana sisi wananchi tunatamani uendelee kukaa mle ndani.

Ukisema kila mtu afanye apendavyo itakuwa mtihani, ndio maana tumeweka utaratibu kuendesha hiki chombo ili wabunge tuheshimiane lakini pia wabunge waheshimu viongozi, lakini pia waheshimu wananchi wao kwa hiyo yote yamewekwa kwa mazingira hayo.

Pengine hamjawahi kuliona, lakini hata mbunge akiwa amevaa namna isivyostahili mle ndani atatolewa. Kwa hiyo haya yote yamewekwa kwa ajili ya kuweka mazingira fulani ya heshima.

Swali: Umekuwa ukiwatoa wabunge nje. Je, toatoa ya wabunge itaendelea?

Jibu: Changamoto inayokuja ni ule upendeleo wa dhahiri hilo ni jambo ambalo haliruhusiwi, lakini kama mtu amefanya kosa anapaswa kuadhibiwa kama ambavyo mwingine aliyefanya kosa kama hilo aliadhibiwa.

Hapa nitatoa mfano mmoja kwa sababu ni kweli pengine ilionekana kwa sababu nilikuwa nakaa mara nyingi pale ndani kwa hiyo ikaonekana huyu ndiye anaye toatoa watu halafu wengine hawatoi.

Huu mfano nimeshautoa mahali pengine, sasa kwa sababu hawa wote wanaohusika ni viongozi sitawataja majina, lakini nielezee tu mazingira.

Siku moja mimi tena nikiwa nimekaa pale mbele mbunge wa Chadema, Bunge lililopita alishika zile taarifa zinazoletwa pale bungeni (sasa hivi tuna vile vishkwambi) zamani tulikuwa tunaletewa kwa karatasi.

Akashika taarifa ya Serikali kwa namna ambavyo inashusha hadhi, hiki ni kitu gani, kama vile ni hali ya kawaida halafu akairusha kwenye kiti cha Spika ambako nimekaa mimi, yaani kuonyesha kwamba huu ni uchafu, hamna hoja yoyote hapa.

Katika kurusha kitabu kile kikachanika, lakini mimi nilichofanya kwa sababu mimi ndiye nilikuwa nimekaa pale mbele niliwaomba watulie kwa kumuomba mbunge akae na kama kukaa hawezi na jengo kama nilivyosema watu 393 utakaa unaongea na mtu mmoja kwa dakika ngapi. Kwa hiyo lazima awapishe ili shughuli zilizopangwa ziendelee.

Sasa yule mbunge alivyofanya hivi hakufukuzwa bungeni. Ikatokea mbunge wa CCM akashika taarifa ya kambi rasmi ya upinzani bungeni, akaishika siku nyingine kabisa, naye akaishika kwa namna ileile kama yule alivyokuwa ameshika, akasema hamna kitu mnaandika ujinga, sijui na mambo kama hayo.

Hawa huku upande mzima wakasimama wakilalamika amechana taarifa ya Bunge. Kwa sababu ikishaletwa pale mbele ni taarifa ya Bunge.

Niliwaambia watulie nifanye maamuzi. Yule aliyeomba mwongozo wa spika ni yule (wa Chadema) aliyerusha kile kitabu wakati ule akitaka huyu wa CCM aadhibiwe kwa dharau alioifanya.

Nikasimama nikasema lakini umesahau kwamba Bunge lililopita wewe ulirusha kitabu huku mbele na kilichanika, kwa huyo alichokifanya usinipangie mimi namna ya kuamua kama nilivyoamua kwenye hoja yako wakati ule ndivyo ninavyoamua kwenye hoja hii wakati huu kwa hiyo hata yeye aendelee kuchangia, lakini hilo aliloifanya si jambo jema kama nilivyokuonya wewe wakati ule.

Kelele zikaendelea nikawaambia basi tokeni nje. Sasa ukishasema tokeni nje watu wanatoka nje ya Bunge halafu watarudi kesho yake.

Kwa hiyo ile toa toa, wakati mwingine kuna kuwa na upotoshaji mkubwa sana na hili niseme wazi, wakati mwingine vyombo vya habari kwa sababu ya ule uchache wao, kwa hiyo utetezi unakuwa hawa lazima wanaonewa.

Swali: Kwa nini majibu ya Serikali kwenye maswali yanayoulizwa na wabunge mara nyingi yanarudiwa yale yaliyotolewa miaka iliyopita.

Jibu: Ni kwa sababu hata sisi wabunge nyakati nyingi huwa tunarejea maswali yale yale, kwa nini kwa sababu uliuliza mwaka jana unaona jambo halijafanyika, umeuliza tena mwaka huu, sasa hana jibu lingine zaidi ya hili la kukujibu.

Hiyo ni ngazi moja, ngazi ya pili ni lile linakuja kama swali la nyongeza. Swali la nyongeza lina changamoto pia.

Kwanini kwa sababu hakuwa ameambiwa ile barabara itaulizwa tena, kwa hiyo unaona utasema hata mwaka jana ulinijibu hivi, lakini kiuhalisia ni kwamba hajapata fursa ya kutafuta majibu mahususi kwa swali lako la nyongeza kwa sababu hakujua utaulizia hiyo barabara yako, kwa hiyo anakujibu yale anayokumbuka.

Hata hivyo, niseme hili ulilouliza pengine ni upungufu ambao ni sehemu ya mambo ambayo tunatakiwa kuyafanyia kazi kwa maana ya kufuatilia yale maswali ya msingi kama jibu limekuja vilevile kwa sababu taarifa sisi kama Bunge tunazo.

Swali: Wabunge wengi ndani ya Bunge wanatoka CCM. Wewe unaonaje ukilinganisha na Bunge lililopita?

Jibu:Nimekuwepo kwenye mabunge yote la 11 na hili la 12, hivyo nimeona namna yanavyofanya kazi. Na mimi ni mbunge wa jimbo. Kwa hiyo uchaguzi huwa una mambo mengi na kwa sababu hili jumba la wawakilishi, maana yake wananchi ndio waliowaleta hawa wawakilishi.

Kwa hiyo huwa napata wakati mgumu sana kwa kuonyesha pengine kuna mahali ambapo hapako sawa ama kuna mahali pako sawa, lakini kwa ujumla namna ya ufanyaji kazi, mimi hutazama wale wananchi huyu waliyemtuma anafanya kazi anayotakiwa kufanya au hafanyi.

Yule ambaye hafanyi ndio maana hapa niliomba kwamba tunahitaji ushirikiano wenu kwa maana ushirikiano kwa wabunge kwenye maeneo yao ya uwakilishi, lakini na Bunge kama taasisi.

Kwa nini nilisema hivyo, nilisema hivyo kwa sababu mbunge hata kama anonekana yuko namna vipi, lakini ndiye waliyemleta wale wananchi kwa hiyo vyombo vya habari tunavitarajia hata kule jimboni kwake vipite pia vikaangalie kuna changamoto gani, kama yeye hazifikishi kwa sababu ya hili na lile, kwa hiyo sote tunategemeana.

Mimi nimeshakuwepo haya mabunge, labda tofauti ni ule munkari ndio haupo. Na munkari siyo uwakilishi wa wananchi sasa hapo mimi nazungumza pia ni mwakilishi wa wananchi kwa sababu hoja zako zitasikika tu, umepiga kelele hujapiga kelele, umeongea kistaarabu au umeongea kwa aina fulani bado hoja zako zitasikika tu.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments