Recent-Post

Kifusi chaua wawili mgodini Chunya

Watu wawili wamefariki dunia baada ya kufukiwa na kifusi cha udongo kwenye mgodi wa dhahabu katika mtaa wa Itumbi mji mdogo wa Makongolosi wilayani Chunya.

Tukio hilo limetokea Februari 11, 2022 ambapo waliofariki ni aliyekuwa mfanyabiashara wa nyama na ndizi, Silivia Chikondo (42) na mwingine ni alikuwa mchimbaji wa madini, Ali Jabiri Bakari.

Wakizungumzia tukio hilo baadhi ya mashuhuda wamesema waliofariki walikuwa wamekaa juu ya eneo la shimo ambapo udongo ulianza kuporomoka na baadaye kuwafukia.

Mmoja wa walioshuhudia, Kiya Mathayo amesema baada ya watu hao kufukiwa walipiga kelele wakiomba msaada, baadaye watu wakakusanyika kufukua lakini udongo huo ulikuwa mwingi.

Mtoto wa Silivia, Regina Peter amesema alikuwa na mama yake katika eneo hilo lakini muda udongo huo ulipokuwa unawafukia yeye alikuwa pembeni.

Mkuu wa Wilaya ya Chunya (DC), Mayeka Mayeka amethibitisha kutokea vifo hivyo huku akiwataka wachimbaji kuwa makini hasa kipindi hiki ambacho mvua zinazoendea kunyesha.

Mayeka ameagiza kusimamishwa shughuli za uchumbaji katika mgodi huo kwa muda ili kupisha uchunguzi.

Wakati huohuo, Mkazi wa Kata ya Mbugani wilayani humo, Anna Mwahalega (58) ameuwawa na watu wasiojulikana.

Dc Mayeka amesema amesikitishwa na unyama aliyofanyiwa mwanamke huyo na kutoa onyo kwa watu wanaofanya matukio hayo.

 

Post a Comment

0 Comments