Madiwani Mbarali kumfuata Rais Samia Ikulu kuomba aunde tume

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya wameazimia kuteua wajumbe watakaoenda Ikulu kuonana na Rais Samia Suluhu Hassan kumuomba kuingilia kati mgogoro wa eneo ilikojengwa shule ya sekondari ya Luhanga ambao unadaiwa kukwamisha wanafunzi 101 kujiunga kidato cha kwanza mwaka huu.

Madiwani hao wamesema kuwa wanataka kutuma wawakilishi kwenda kumuomba mkuu wa nchi kuunda tume huru ambayo itafanya tathimini ya eneo hilo ili kuruhusiwa kuendeleza shule hiyo.

Eneo hilo ambako imejengwa shule ya sekondari ya Luhanga linadaiwa kuwa eneo la hifadhi ya Ruaha hivyo kulazimu kusimamishwa kuendelezwa shule hiyo ambayo mpaka sasa ina vyumba vinne vya madara.

Katika eneo hilo ndipo lilipowekwa jiwe la GN 28 ambalo ni alama ya kutenganisha makazi na hifadhi ya Ruaha.

Shule hiyo ambayo imejengwa kwa nguvu za wananchi ilikuwa iwe suluhu kwa wanafunzi wanahitimu darasa la saba na kufaulu, ambao kwa sasa wanatembea zaidi ya kilometa 10 kwende kujiunga shule ya sekondari ya Utengule ambayo ipo kata ya jirani.

Kutokana na umbali huo, wanafunzi 18 pekee kati ya 119 waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule ya sekondari ya Utengule ambao walifaulu darasa la saba katika shule ya msingi Luhanga ndio walioripoti mpaka sasa tangu masomo kuanza Januari 17 huku 101 wakiwa hawajaripoti.

Wakizungumza kwenye kikao cha Baraza la kawaida la Madiwani kilichofanyika leo Februari 12, 2022 wamesema kuwa wamefikia hatua hiyo ya kuteua wajumbe kwenda kuonana na Rais Samia kutokana na mgogoro huo wa muda mrefu kati ya vijiji vinavyozunguka kata ya Luhanga kudaiwa kuwa ndani ya eneo la hifadhi na kupelekea kukwama kwa mradi wa shule ya sekondari ya kata hiyo ambayo ilijengwa miaka mitano iliyopita.

Wamesema kuwa baada ya kutembelea eneo hilo wameona linafaa shule hiyo kuendelezwa hivyo wameazimia kutuma wajumbe kuonana na Rais Samia kumuomba ateue tume itakayofanya tathimini ya eneo hilo ambalo pia linadaiwa kuwa kwenye mkondo wa maji.

Diwani wa Kata  Igava, Udessy Nassoro amesema kitendo cha  kata  hiyo  kukosa shule ya sekondari  kunapalekea wanafunzi wanaochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza kukosa haki zao za msingi za kupata elimu huku baadhi wakiishia kupata mimba za utotoni na wengine kuchunga mifugo.

''Mwaka huu watoto waliochaguliwa ni 119 na mpaka sasa wanaoendelea na masomo ni 18 huku 101 wako majumbani jamani kama madiwani tunatengeneza nini hapo kwa kizazi kijacho naomba kupitia kikao hiki tutoke na majibu''amesema.

Kauli hiyo ambayo imeungwa mkono na madiwani akiwepo Mwenyekiti wa Halmashauri, Twalib Lubambamo na kuongezea kuwa watateua wawakilishi kwenda kumuona Rais Samia na kumuomba kuunda tume huru kuja kufanya uchunguzi kwa madai kuwa tume zilizopita hazikufanya tathimini vizuri ya maeneo yaliyoathirika na jiwe namba 28.

''Jiwe la GN 28 limekuwa kikwazo kikubwa kwa wananchi wilayani Mbarali hususani kwa vijiji vinavyozunguka kata ya Luhanga watoto wanaacha masomo kutokana na umbali wa shule huku kwa mwaka jana pekee 120 waliacha masomo''amesema.

Ameongeza kuwa kutokana na mvutano wa mipaka kama uongozi walifika kujiridhisha na kuona kuna kila sababu Rais kuunda Tume nyingine kuchunguza kwani kuna uwezekano taarifa zilizopelekwa mezani kwake sio sahihi.

Lubambamo amesema kuwa wamepeleka Sh1 milioni katika shule ya sekondari Luhanga kukkarabati matundu ya vyoo ili wanafunzi hao 101 waweze kuanza masomo kwa muda kwenye shule hiyo.

''Kwa sasa ili kuokoa watoto 101 kuendelea na masomo kama halmashauri kuna fedha kama milioni moja tumepeleka katika Shule ya Sekondari Luhanga kwa ajili ya kukarabati wa matundu ya vyoo  ambako watasoma kwa muda huku tukisubiri kauli ya Rais mara baada ya madiwani kukutana naye na kufanya mazungumzo''amesema.

Katibu wa Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbarali, Richard Kilumbo ameagiza zifanyike jitihada za haraka kuhakikisha wanafunzi hao kuanza masomo mara moja katika kulinda Sera na Katiba ya nchi katika suala la elimu.

''Naagiza mkae na nipate mrejesho kuhusiana na watoto 101 ambao hawajaripoti shule mpaka sasa pia zungumzeni na wazazi kuhusiana na utaratibu zinazofanywa kuhusiana na migogoro wa jiwe namba 28 baina ya wananchi na hifadhi'' amesema

Diwani wa Kata ya Luhanga, Baraka Lateo amesema kuwa licha ya watoto hao 101 kutoripori shule kwa mwaka huu lakini mwaka jana wanafunzi 120 ambao walikuwa wanasoma Utengule wakitokea kata ya Luhanga waliacha masomo kutokana na umbali.

''Tunaomba busara ya Rais Samia Suluhu itumike kwani wananchi hawa asilimia kubwa ni jamii ya wakulima na wafugaji na kumekuwepo ba mikwamo ya miradi mingi ya maendeleo sababu kubwa ikiwa ni jiwe namba 28’ amesema.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments