Mkutano wa viongozi wa Umoja wa Afrika na wa Umoja wa Ulaya umeanza leo katika mji mkuu wa Ubelgiji Brussels. |
Viongozi hao wanakutana kwa ajili ya mazungumzo ya siku mbili kuanzia leo, wakiazimia kuimarisha ushirikiano, huku Ulaya ikiahidi uwekezaji mkubwa barani Afrika.
Mkutano wa mara hii una umuhimu wa aina yake kutokana na changamoto mbalimbali zinazolikabili bara la Afrika na mataifa ya Ulaya pia. Akihutubia katika mkutano huo, Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa, bara la Ulaya linapaswa kuisaidia Afrika ili kuyashughulikia matatizo yake.
Uhusiano baina ya mabara hayo mawili umekuwa ukiingia dosari kutokana na matatizo mtawalia, yakiwemo usambazaji wa chanjo ya Covid-19, namna ya kuzuia uhamiaji haramu, wimbi la mapinduzi ya kijeshi barani Afrika na kadhalika Rais wa Senegal Macky Sall ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika amesema lengo la mkutano huu ni kufikia uhusiano mpya unaodhihirika kwa vitendo.
Katika miaka ya hivi karibuni, uhusiano wa Bara la Afrika na Umoja wa Ulaya umekumbwa na changamoto na hata mivutano tofautio kuhusiana na masuala mbaliambali.
Viongozi wa Afrika wamekuwa wakikosoa sera za baadhi ya mataifa ya Umoja wa Ulaya kwa bara la Afrika huku baadhi ya mataifa hayo yakiamiliana na nchi za Kiafrika kama koloni lao.
0 Comments