MOHAMED SAID: Alifungwa wakati wa Nyerere, asamehewa wakati wa Rais Samia


 Usiku wa Februari 24 mwaka 1982 utabaki kwenye kumbukumbu ya kudumu kichwani kwa Mohamed Said (70) kutokana na tukio kubwa lililomkuta siku hiyo na kumfanya akae gerezani kwa miaka 40.

Kama angejua kinachokwenda kumtokea siku hiyo huenda angebadilisha mwelekeo, lakini kwa kuwa hakutambua alijikuta akifuata starehe iliyokatisha uhuru wake akiwa kijana na kurejeshewa tena uzeeni muda mrefu ukiwa umeshapotea.

Mzee huyu aliyeingia gerezani akiwa kijana wa miaka 30 na kutoka akiwa na miaka 70 ni miongoni mwa wafungwa waliopata msamaha wa Rais Samia Suluhu Hassan mwishoni mwa mwaka jana wakati maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru.

Mwananchi limefunga safari hadi Chamazi, Dar es Salaam kukutana na mzee huyo ambako amepata hifadhi baada ya kutoka gerezani na kukuta hana ndugu yeyote uraiani huku wanafamilia wake wengi wakiwa wameshaaga dunia.

Mohamed, ambaye alikuwa askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) akifanya kazi ya kuangalia usalama kwenye ghala la chakula la jeshi, alikutana na tukio saa chache baada ya kumaliza majukumu yake na kwenda uraiani kwa ajili ya kujiburudisha.

Akiwa amevaa kiraia na begi lake dogo alilohifadhi silaha na vitambulisho vyake, alitoka kazini kwake Lugalo na kwenda kupumzisha akili Manzese kabla ya kurejea nyumbani kwake Mwenge.

Huko Manzese alikwenda kwenye baa maarufu wakati huo ilikuwa ikifahamika kama Matunda Bar ambapo aliweka begi lake mezani na kuanza kupiga kinywaji.

Kwa kuwa eneo hilo alikuwa mwenyeji hakuna na wasiwasi na kile alichoweka kwenye begi, aliendelea kunywa na kuna wakati alinyanyuka kwenda msalani na hata aliporudi hakuwa na wazo la kuangalia begi lake kama lipo.

“Ilipofika saa tatu na nusu kuelekea saa nne nikaona sasa pombe imeshatosha, niondoke zangu kurudi nyumbani, hapo ndipo nikapata akili ya kuangalia begi langu pale mezani sikuliona, nilishtuka na kitu cha kwanza kuwaza ni kuhusu ile silaha, pili ndani ya lile begi kuna vitambulisho vyangu, jambo hili lilinifanya nichanganyikiwe.

“Nilijaribu kutafuta pale kwa muda bila mafanikio, nikiwauliza niliokaa nao wanasema hawajamuona mtu aliyechukua begi na huwezi kumuwajibisha muuzaji ilibidi nirudi kambini, kule nilipoelezea mazingira ya tukio zima ikabidi niende polisi kutoa taarifa, huko nikakuta tayari taarifa zangu zimefika askari wananigeuzia kibao na kuniambia mimi ni mhalifu.

Hilo lilitokana na vitambulisho vyake kukutwa pamoja na silaha iliyotumika kwenye tukio la wizi wa gari na mauaji.

Kadiri alivyojaribu kuelezea kuwa silaha yake iliibiwa, hivyo hausiki na tukio hilo hakueleweka na hatimaye akawekwa chini ya ulinzi na rasmi akabadilika jina kutoka kuwa askari hadi mtuhumiwa.

Alikaa kituoni hapo kwa takribani siku saba ndipo alipopelekwa mahakamani kwa mara ya kwanza na kesi kuanza kutajwa akiwa na wenzake watatu waliokamatwa na kuhusishwa na tukio hilo.

Kupelekwa kwake mahakamani kukamfanya kupelekwa katika gereza la Keko kama mahabusu ambako alikaa kwa miaka 10 kabla ya kuhukumiwa rasmi na kuanza kutumikia adhabu yake.

Anasema tofauti na ilivyo sasa ambapo kesi zinaendeshwa ndani ya muda mfupi, wakati huo rushwa ilikuwa ikitumika kuchelewesha upelelezi hivyo, walijikuta wakisota kwa muda mrefu kwa sababu kuna wengine waliohusishwa na kesi hiyo walikuwa nje.

Katika kipindi chote cha miaka 10 aliyokuwa mahabusu bado aliendelea kuhesabika kama mwanajeshi na akapandishwa cheo kuwa sajenti akiendelea kupata stahiki zake zilizoelekezwa kwa familia yake hadi pale alipohukumiwa ndipo ilipokoma rasmi.

“Kesi ilitajwa kwa muda mrefu kabla ya kuanza kusikilizwa, hivyo tuliendelea kusota mahabusu hadi pale iliposikilizwa na hatimaye baada ya miaka 10 ikaonekana tuna hatia. Nakumbuka ilikuwa Mei 20 mwaka 1992 ndiyo hukumu yetu ilitoka tukahumumiwa kunyongwa.

“Siku hiyo ilikuwa ngumu mno kwangu, moyoni nilikuwa kama nimechomwa na msumari wa moto yaani najua kabisa sihusiki, lakini nakumbana na adhabu kali namna hii. Ile sauti ya kwamba wamehukumiwa kunyongwa ilikuwa ikijirudia masikioni mwangu, sikuamini kwamba hili linanikuta mimi.

“Wazazi wangu walipatwa na mshtuko, hawakutegemea kama ningekutwa na jambo zito kama hilo, sikuwa na la kufanya nikamuomba Mungu anipe moyo wa ujasiri kuweza kukabiliana na hilo kwa kuwa niliamini kwa akili na nguvu zangu mwenyewe siwezi.”

Si yeye wala wenzake wawili waliokubaliana na adhabu hiyo, hivyo wakafikia uamuzi wa kukata rufaa, hilo likafanyika kwa haraka na wakawasilisha maombi yao kunakohusika.

Baada ya kuhukumiwa, Mohamed akapangiwa kwenda gereza la Ukonga kusubiri siku ya adhabu kama ilivyoamuriwa huku kichwani mwake akijua kinachofuata ni kunyongwa.

Pamoja na ukweli huo bado alikuwa na matumaini ya rufaa waliyokata ambayo hata hivyo haikuwa na matokeo chanya kwa wote, mmoja ndiye aliyeshinda na kuachiwa huru.

Hivyo gerezani wakabaki wawili hapo ndipo alipotambua na kukubaliana na ukweli kuwa hayo ndiyo makazi yake rasmi hadi pale utekelezaji wa adhabu yake utakapofanyika.

Maisha mapya baada ya kuhukumiwa

Akiwa gerezani alijitahidi kuwa mtiifu na kushirikiana na wafungwa wenzake kwa kila hali na akifuata maelekezo ya askari magereza huku akijiweka zaidi karibu na Mungu akiamini yeye ndiye anayejua hatima yake.

“Kiukweli ilifika wakati nikaona sina uwezo wa kufanya chochote nimuachie Mungu, nijiweke karibu zaidi naye anijalie afya njema wakati wote nikiwa pale gerezani na hata akiamua kunichukua, niwe katika mazingira mazuri. Nilikuwa nasali na kitu msichojua kule watu wanasali mno yaani uwepo wa Mungu upo kwa kiasi kikubwa,” alisema. Je nini kilitokea wakati akiwa gerezani kusubiri hukumu yake ya kunyongwa? Fuatilia kesho.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments