Naibu Waziri aeleza jinsi sheria ya makosa ya mtandao inavyoweza kuwafunga watu

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mathew Kundo amesema kama Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 ingetumika kama inavyotakiwa, mahabusu zingejaa.

Kundo ameyasema wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo maofisa upelelezi wa Jeshi la Polisi nchini juu ya sheria.

“Sheria ya Makosa ya Mtandao kama ikitumika kama ilivyo, tutajaza mahabusu. Hivi unajua uko ofisini ukiambiwa kutumia kompyuta yako hadi saa 10:00 ukitumia hadi saa 10.02 utakuwa umeingia katika cybercrime (makosa ya kimtandao),” amesema.

Amesema maana yake ni kwamba mtu ametumia bila kuruhusiwa kwa kuzidisha muda wa matumizi wa kompyuta yake. Amewataka maofisa hao kwenda kuisoma vizuri sheria hiyo.

“Tunafahamu confusion (mkanganyiko) kati ya ofisi ya DCI (Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai) na TCRA, there is a lot of confusion (kuna mkanganyiko mkubwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano-TCRA),” amesema.

Kundo amesema mkanganyiko huo unawafanya wananchi wanapokamatwa kwa makosa ya kimtandao kudhani kuwa amekamatwa na TCRA. Amesema sheria hiyo inasimamiwa na Jeshi la Polisi kupitia kwa Mkurugenzi wa Upelelezi (DCI).

Amesema kuna changamoto nyingine zinatokana na watumishi na nyingine zinatokana na vitendea kazi na kwamba hizo zote zinatakiwa kuangaliwa.

“Tukiwa tunamchapa ng’ombe kuwa hatoi maziwa lazima tuhakikishe kuwa tumempa chakula…lakini mazingira katika uadilifu nimeyasikia katika wimbo (wa polisi) wenu na mmeimba vizuri sana na nimeupenda. Nendeni mkatafsiri wimbo huo katika uhalisia,” amesema Naibu Waziri huyo.

Amewataka kutoa elimu kwasababu mazingira ya mwaka 2010 yamebadilika sana hivyo kuna haja ya kukumbushana majukumu yao.

Kundo amesema vita iliyopo duniani hivi sasa si ya mitutu ya bunduki bali ya mitandao na kwamba vita hiyo ni mbaya kwasababu unaweza ukakaa ukidhani uko salama kumbe vitu.

Amesema ndio maana inatakiwa kuwa na kitengo cha intelejensia ambacho kina nguvu inayoendelea kuboreshwa zaidi.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments