NAIBU WAZIRI GEKUL AELEZA MIKAKATI YA KUKUZA RIADHA KILI MARATHONI

    


Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Pauline Gekul amewapongeza waandaji wa mbio za Kilimanjaro Marathoni huku akifafanua kwamba tukio hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Michezo nchini inayosisitiza ushiriki wa pamoja kati ya Serikali na wadau katika kuendeleza michezo mbalimbali ikiwemo riadha.

Mhe. Gekul ameyasema hayo leo Februari 27, 2022 wakati akimkaribisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) ili atoe hotuba yake kwenye kilele cha mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon, 2022 kwenye viwanja vya Chuo kikuu cha Ushirika Moshi.

“Sisi familia ya michezo tunajivunia uwepo wa tukio kubwa namna hii linalowaleta pamoja wanamichezo na wapenzi wa riadha kutoka katika maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi yetu, kipekee niwapongeze Kilimanjaro Premium Lager kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukuza michezo hapa nchini”. Amesema Mhe. Gekul.

Amesema katika kuhakikisha Serikali inaibua na kuendelea vipaji vya michezo ikiwemo mchezo wa Riadha, Serikali imeandaa Mpango Mkakati wa Utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Michezo nchini.

Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kusaidia maandalizi na ushiriki wa timu za Taifa zikiwemo timu za riadha katika mashindano mbalimbali ya Kimataifa na kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Shilingi Bilioni 1.5 zimetengwa.

Amefafanua kuwa Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya Michezo na mwaka wa fedha 2021/2022 kiasi cha Shilingi Bilioni 10.5 kimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Michezo (Sports Centres) katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Geita na kwamba vituo hivyo vitakuwa ni kichochezo kikubwa kwa vijana wetu kushiriki katika michezo.

Pia, amesema Wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Wizara ya TAMISEMI wameendelea kuratibu michezo ya Shule za Sekondari na Msingi (UMISSETA na UMITASHUMTA), pamoja na kuteua na kuendeleza Shule 56 za Michezo na amesisitiza kuwa Mkakati huo utasaidia kuibua vipaji vya michezo shuleni ikiwa ni pamoja na kuvilea na kuviendeleza vipaji hivyo. Aidha, Mhe. Majaliwa ametoa maelekezo makubwa matatu kwa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na ameitaka kushirikiana na Wizara ya Maliasili Utalii na muandaaji Executive Solution kuona namna bora ya kuandaa tamasha hili kwa miaka ijayo ili kuwaleta watalii wengi pamoja na kuongeza siku na wadau.

Wizara kushirikiana na Shirikisho la Riadha nchini kuandaa kalenda ya mwaka mzima ya mbio nchi nzima na kuandaa vikao vya wadau wote wa riadha nchini ili kupate mawazo ya kuendesha tamasha hili ili liwe na sura ya kimataifa.

Mbio za Kilimanjaro Marathoni za mwaka huu ni za 20 toka kuanzishwa kwake ambapo zimehusisha Kilomita 42, 21 na kilomita tano huku zikiwa na washiriki wengi zaidi kuliko miaka yote ambapo zaidi ya wakimbiaji 12000 wameshiriki kutoka nchi 56 duniani.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments