NGORONGORO IPO HATARINI KUPOTEA, RIPOTI YA AWALI YAFICHUA YASIYOSEMWA

 NGORONGORO inateketea au hali ni mbaya Ngorongoro ndivyo unaweza ukasema kutokana na sababu mbalimbali zinazoashiria kuharibiwa na hatimaye kupotezwa kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, hifadhi yenye sifa lukuki ndani na nje ya nchi.

Ongezeko katika hifadhi hiyo ambapo limeongezeka maradufu kutoka watu 8,000 mwaka 1959 wakati wanahamishwa kutoka Serengeti hadi zaidi ya watu 110,000 linasababisha madhara makubwa yanayopelekea kupotea kwa uhifadhi na madhara makubwa kwa wakazi wenyeji.

Kituo cha Wanahabari Watetezi wa Rasilimali na Taarifa (Media Centre for Information and Resources Advocacy - MECIRA) kimesikitishwa na hali ya maisha duni wanayoishi wakazi wa Tarafa ya Ngorongroro iliyopo ndani ya hifadhi kutokana na uduni wa maisha unaotokana na changamoto kadhaa kubwa ikiwa ni kuongezeka kwa kasi kwa idadi ya watu ndani ya eneo hilo la hifadhi kunakosababisha kuongeza umaskini kwa wakazi husika.
Katika taarifa yao kwa vyombo vya habari iloyosainiwa na mkurugenzi mwendeshaji wa kituo hicho, Habibu Mchange, wamesema kuwa tatizo lililopo Ngorongoro haliathiri uhifadhi pekee bali pia hata maisha ya wananchi wa eneo hilo wanaathirika kutokana na ongezeko kubwa la watu kuliko uwezo wa eneo kuwahudumia.

Mchange amewataka wanaharakati wote wanaojitokeza kupaza sauti, kuhakikisha wanasimama kwenye ukweli ili kuwanusuru wakazi wa eneo hilo ambao kwa hakika usalama wao kiuchumi, kiafya, kielimu na kiusalama ni mdogo sana kutokana na wingi huo wa watu.
‘’Utafiti wetu tulioufanya kwa wiki mbili tatu hizi, pamoja na kupitia nyaraka mbalimbali, taarifa mbalimbali na mazungumzo baina yetu na wakazi wa eneo husika, tumebaini kuwa mambo mengi yanayosemwa na wanaharakati kadhaa na kuripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari hayana ukweli na kwa kweli yanapotosha umma na wakazi wa eneo husika hayawapendezi.

‘’Kwa kweli tumegundua mambo mengi sana, tumegundua namna watoto wadogo wa Kimasai wanavyotumikishwa kazi ya ufugaji kutwa nzima bila kujali kama kuna kwenda shule, tumegundua namna maradhi ya milipuko yanavyowatesa wakazi hawa, tumegundua namna umaskini ulivyokithiri kiasi ha watu zaidi ya asilimia 50 kuwa katika hali kubwa ya umaskini licha ya kuwaona wamezungukwa na mifugo mingi.

‘’Taarifa zinasema mwaka 1959 palikuwa na watu chini ya 8000 tu, emagine mwaka 2017 watu walifika 94,000, leo hii wanakadiriwa kufika watu laki moja na elfu kumi na kidogo, kwa ukuaji huu wa watu kuna kila sababu ya watu hawa kutafutiwa maeneo huru ya kuishi ili waweze kujiendeleza bila kuathiri uhifadhi na mazingira, mle hifadhini kwa sheria inayosimamia uhifadhi hawataweza kupata haki yao ya maendeleo endelevu, hivyo watakuwa masikini tikatika jambo ambalo linawezekana kabisa kuepukwa kwa wao kuondoka,"ananukuliwa Mchange katika taarifa yake hiyo.
Mchange anasema kuwa hadi sasa taarifa za NBS zinaonesha kuwa pamekuwepo na hali ya kudumaa kwa uchumi ambapo zaidi ya kaya 5,000 kati ya kaya 22,000 (22%) zilizopo hifadhini humo hazina mifugo.

"Tunajiandaa kutoa taarifa rasmi ya uchambuzi wa hali ilivyo, ilivyokuwa na itakavyokuwa hivi karibuni, lakini kwa sasa sisi kama MECIRA pamoja na kutishwa kwetu kwa kuathirika kwa hali ya uhifadhi ya mamlaka ya Ngorongoro, tunadiriki kusema kuwa hali pia ya maisha ya wenyeji ni mbaya pengine kuzidi maeneo mengi hapa nchini, na ubaya huu unatokana na kuongezeka kwao kwa kasi kubwa,"imeongezeka.

Taarifa zaidi zilizoifikia DIRAMAKINI BLOG zinaonesha kuwa miaka kadhaa nyuma zilihamishwa kwa hiyari zaidi ya kaya 110 kutoka hifadhini kwenda Kijiji cha JEMA kilichopo wilayani humo.
Hivi karibuni iliripotiwa kuwa Hifadhi ya Ngorongoro ipo hatarini kupotea na kupoteza uhai na umashuhuri wake kutokana na kukithiri kwa shughuli za kibinadamu ikiwemo ufugaji uliopitiliza kiasi, ujenzi wa nyumba zisizofuata taratibu za kihifadhi na shughuli nyingine za kibiashara.

Mwandishi wa habari hizi ameshuhudia makundi makubwa ya mifugo ikiwemo ng’ombe, mbuzi, kondoo, punda, kuku, na mingineyo ikichukua eneo kubwa kuliko wanyama wa asili wanaopendwa kufuatiliwa na watalii.

Pamoja na kuzingatia ukweli kuwa Ngorongoro ni hifadhi ya kipekee inayowahusisha wanyama binaadamu na mifugo kwa pamoja, lakini hali ilivyo kwa sasa inatisha kiasi cha kutishia usalama wa hifadhi na wananchi husika wa asili wanaoishi katika eneo hilo.
Taarifa za uhakika ambazo zimepatikana ni kuwa mwaka 1959 wakati wakazi walioruhusiwa kuishi katika hifadhi hiyo kwa mchanganyiko wao na Wanyama pori, wakazi hao hawakuzidi watu elfu tisa tofauti na sasa wakazi hao wamefika zaidi ya laki moja na mifugo yao wanayoimiliki ikikadiriwa kuwa zaidi ya laki sita.

‘’Kwa mujibu wa taarifa wanasema kuna mifugo laki mbili na nusu, nadiriki kusema sio kweli, mifugo hii haipungui laki saba hadi laki nane…hebu angalia tangu tumeanza makundi ya ng’ombe, mbuzi na kondoo sasa hivi ni zaidi ya saa mbili tunazunguka tunawaona tu…hii maana yake ni kwamba hata kama watu hawa wapo kisheria, lakini inahitajika jitihada za makusudi kunusuru tatizo hili…hili ni tatizo kwa kweli,"amesema Paul Schenzern raia wa Ujerumani aliyekuwa katika safari za kitalii.

Schezern ameongeza kuwa, kwao wanavyoifahamu Ngorongoro ni kwamba ni eneo bora zaidi la kiutalii na kamwe hakuwaza kama angepita barabani akipishana na ng’ombe na mifugo mingine japokuwa alikuwa anaufahamu kuwa Ngorongoro wanaishi binadamu na wanyama lakini si kwa kiwango alichokiona.

‘’Nimetembea hifadhi kadhaa Duniani ambazo Wanyama na binaadamu wanaishi kwa asili, kwa kweli zinavutia n ahata kuishi kwao kunaemndana na uhifadhi wa mazingira, tofauti na hapa Ngorongoro…nitapata shida sana kumshawishi mtu atakayeniomba ushauri juu ya kutaka kuja hapa. Nafikiri watetezi wa haki za binadamu, mifugo, wanyama na mazingira wanapaswa kupaza sauti ya pamoja kuinusuru hifadhi hii muhimu na bora.

‘’Unajua watu wanaweza kulalamika kwamba wanaishi humu na haipaswi kupangwa vizuri, lakini sio sahihi watetezi makini wa binadamu wanatakiwa watetee kwanza usalama wa mazingira, usalama wa mazingira ya Ngorongoro ndio usalama wa Arusha, usalama wa Arusha ndio usalama wa Tanzania na ndio maana Dunia nzima kunakuwa na sheria kali zinazolinda mazingira...kujazana kwa watu na mifugo hifadhini sio haifai tu kwa mifugo bali haifai zaidi kwa binadamu wanaoishi humo kwani kuishi kwao kunategemea zaidi ikolojia ya hifadhi husika,’’ameongeza.

Wakati huo huo, Mchange alisema kuwa hata yeye alikuwa Ngorongoro mwishoni mwa mwaka jana na ameshuhudia ujenzi uliokithiri na unaovunja kabisa sheria na kanuni za uhifadhi na kuongeza kuwa anaandaa ziara ya wanahabari wanarasilimali asilia na taarifa kwenda kujionea hali ilivyo na kuuhabarisha umma na kuwataka wanaharakati kushirikiana kuokoa kivutio hicho muhimu.
'’Hata mimi nilitembea tembea mwishoni mwa mwaka, niliyoyaona Ngorongoro kwa kweli yanatisha na hayafai kusimuliwa hata kidogo, wadau wa utalii, uhifadhi na mazingira tusipochukua hatua na kupaza sauti, Ngorongoro itapotea kama upepo…kwa kifupi tu nikuambie ndugu mwandishi kuwa NGORONGORO IPO HATARINI KUPOTEA,"aliongeza Mratibu Mchange.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments