Ni fungua ukurasa ya siasa nchini

Ni “fungua ukurasa”. Maneno haya mawili ndiyo yanayochomoza katikati ya maoni ya wasomi na wanasiasa kuhusu mkutano wa Rais Samia Suluhu Hassan na Tundu Lissu jijini Brussels, Ubelgiji.

Rais Samia na Lissu ambaye ni makamu mwenyekiti wa Chadema walikutana juzi na kufanya mazungumzo takriban kwa saa moja, jambo lililoibua mjadala ndani na nje ya nchi, likitafsiriwa kuwa mwanzo mpya wa siasa za demokrasia nchini.

Rais Samia yuko nchini humo kwa ziara ya kikazi wakati Lissu akiishi huko baada ya kupata hifadhi wa kisiasa, kwa alichoeleza ni wasiwasi juu ya maisha yake.

Taarifa iliyotolewa Ikulu haikuweka bayana yaliyozungumzwa, lakini Lissu alibainisha kupitia mitandao ya kijamii mambo aliyomweleza Rais Samia, ikiwamo kesi ya mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Mambo mengine alisema ni zuio la mikutano ya hadhara, suala la katiba mpya, mafao yake ya ubunge na suala la usalama wake na makada wengine wa Chadema walioko uhamishoni ikiwa watarejea nchini.

Hata hivyo, Rais Samia alipohojiwa na Sauti ya Ujerumani (DW), alisema linapokuja suala la ubinadamu anakutana na Lissu kama mdogo wake lakini wakienda kwenye siasa linakuwa suala la kazi, kila mtu anasimama upande wake.

“Kama unakumbuka Tundu Lissu alilazwa Nairobi, mimi nilikwenda kumuona in a very friendly manner, kama dada, nilikwenda nikamwona na tukazungumza vizuri tu. Sasa inapokuja kwenye ubinadamu, Tundu Lissu ni mdogo wangu tu, atakuja tutazungumza, ana shida zake za kisiasa, tutazungumza,” alisema Rais Samia katika mahojiano yaliyorekodiwa kabla hawajakutana.

“Lakini sasa tunapoingia kwenye siasa, huko sasa ni upande wa kazi, yeye atasema ya kwake, mimi nitasimama kwenye chama changu, yeye atasimama na cha kwake, lakini kwa leo anakuja kibinadamu tu kunisalimia, tuonane, nimuone, nisikie anasemaje.”

Alipoulizwa endapo hatua hiyo imekata kiu ya Chadema ya kutaka kukukutana Rais, Katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika alisema hawezi kuzungumzia hilo kwa sasa, bali anukuliwe kwa aliyoyaandika kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Huko Twitter, Mnyika ameandika kwa mtindo wa maswali, “Ukurasa mpya? New chapter? New era? Zama mpya? Mwanzo Mpya? Kitabu kipya? Nawaombeni tujitokeze kesho (leo) 18/02/2022 mahakamani.”

Ingawa hakufafanua, leo ndio Mahakama Kuu imepanga kutoa uamuzi wa iwapo Mbowe na washtakiwa wenzake watatu wana kesi ya kujibu au la.

Licha ya msimamo huo, wasomi wa siasa na wanasiasa wameeleza kwamba kitendo cha wawili hao ni jambo jema na linakwenda kufungua ukurasa mpya wa siasa za Tanzania na matokeo yake yataonekana hivi karibuni.


Jambo jema

Akijadili hatua ya wawili hao, Dk Paul Loisulie, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma alisema ni jambo jema na ilikuwa ni fursa ya kila upande kuonana na mwingine kuzungumzia changamoto za kisiasa.

Alisema ajenda alizotaja Lissu kuwa ameziwasilisha mbele ya Rais zimekuwa ndiyo wimbo wake kila siku, kwamba haki inahitajika katika siasa na kwamba hiyo ilikuwa fursa nzuri ya kuelezea mambo aliyodhani ni muhimu kwake binafsi na kwa siasa za Tanzania.

“Hii inakwenda kufungua ukurasa mpya katika siasa za Tanzania. Kwa vyovyote vile lazima kutakuwa na mabadiliko yatatokea na ni mabadiliko chanya,” alisema Dk Loisulie.

Moja ya mambo yatakayotokea, msomi huyo alisema ni umoja katika nchi, kwamba wananchi wameunganishwa pamoja licha ya tofauti zao za kiitikadi, sasa wana matumaini na hawatakuwa na shida na Rais.

Profesa Abdallah Safari, mwanazuoni wa sheria, siasa na diplomasia, alisema hilo ni jambo jema kwa sababu hata kama wanapingana lazima wakutane kuzungumzia tofauti zao na kuzimaliza.

“Ni kitu kizuri wamekutana, ni kitu positive (chanya) sana kwa sababu wamezungumza matatizo ya hapa, yake Lissu binafsi na matatizo ya demokrasia na kesi ya Mbowe… hizo ni ajenda kubwa nafikiri,” alisema Profesa Safari.

Kwa upande wake Ado Shaibu, katibu mkuu wa ACT Wazalendo alisema majeraha ya demokrasia yaliyojitokeza katika kipindi cha miaka sita iliyopita yanaweza kuponywa kwa mazungumzo.

Alisema Rais Samia aliponyoosha mkono wa mazungumzo, ACT Wazalendo iliitikia hadharani kwamba iko tayari kwa mazungumzo hayo.

“Jitihada zozote, za mtu yeyote yule kuelekea kwenye mazungumzo tunaziunga mkono. Faraja ni kwamba ingawa mazungumzo hayo yalikuwa ya faragha, yale yaliyotajwa na Lissu ndiyo yaleyale ambayo wadau tuliyazungumza Dodoma, kwa hiyo tunaona ni jambo ambalo linaleta faraja,” alisema.

Wakati wasomi na wanasiasa wakiwa na mtazamo huo, Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kimesema mkutano huo ni muhimu katika kujenga maridhiano ya kitaifa na kuwezesha kufanyika kwa siasa kwa manufaa ya wananchi.

“Mkutano huo utarahisisha kazi za kituo kama jukwaa muhimu la majadiliano ya kisiasa katika kuchochea matokeo chanya ya kuweka uwanja sawa wa ushindani wa kisiasa nchini,” inaeleza taarifa ya TCD iliyotolewa na Bernadetha Kafuko, mkurugenzi mtendaji,


Nimemwambia matano

Akizungumza moja kwa moja kupitia mitando ya kijamii baada ya mkutano huo, Lissu alisema amemweleza mkuu wa nchi kwamba kesi inayomkabili Mbowe na wenzake haina manufaa yoyote kwake, kwa chama chake wala kwa Taifa kwa jumla.

“Nimemwambia Rais wetu, hiyo kesi haiisaidii nchi yetu, haiisaidii.... badala yake inamuumiza mwenyekiti wetu na familia yake, inawaumiza walinzi wake na familia zao.

“Nimemwambia Rais afanye analoweza kufanya kwa mamlaka yake kama Rais, ahakikishe kwamba hii kesi inaondolewa mahakamani, hakuna sababu yoyote ya kuendelea na kesi hiyo...” alisema Lissu.

Hata hivyo, Rais Samia alipoulizwa kuhusu kesi hiyo na DW alisema hilo liko mahakamani iachwe itoe maamuzi yake.

Vilevile, Lissu alisema amemweleza Rais Samia kuhusu zuio la vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara na maandamano na amemwomba afute katazo hilo ili sheria ifuatwe.

Pia, alisema amemweleza Rais kuhusu suala la katiba mpya akimwambia kwamba ana fursa ya kuipatia Tanzania katiba mpya na mfumo wa kidemokrasia utakaotenda haki hasa kwenye uchaguzi.

Jambo jingine alisema ni kuhusu haki zake alizonyimwa baada ya kuvuliwa ubunge na amemwomba Rais ashughulikie hilo kwa maana yeye ni mbunge pekee ambaye hakupokea kiinua mgongo chake.

Vilevile, Lissu alisema amemweleza mkuu wa nchi azma yake ya kutaka kurudi nchini na kuwa amemwomba amhakikishie usalama wake na wa viongozi wengine wawili wa Chadema, Godbless Lema na Ezekia Wenje walioko uhamishoni Canada na kuwa Rais alimwambia atalifanyia kazi.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments