Recent-Post

Rais Samia alia na kukwama miradi Mara

Rais Samia Suluhu Hassan amesema Mkoa wa Mara una tatizo la kukwama kwa miradi jambo ambalo linahitaji kupatiwa ufumbuzi.

Ametoa kauli hiyo leo Jumapili Februari 6, 2022 kwenye hafla ya uwekaji jiwe la msingi mradi wa maji wa Mugango- Kiabakari wilayani Musoma huku akiahaidi kuzungumzia suala hilo katika mradi wa ujenzi wa hospitali ya rufaa ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere maarufu Kwangwa.

Mkuu huyo wa nchi ametolea mfano wa miradi iliyokwama kwa muda mrefu kuwa ni pamoja na hospitali hiyo ya rufaa iloyoanza kujengwa mwaka 1974 pamoja na mradi wa umwagiliaji wa Bugwema uliopo wilaya ya Musoma.

Mkoa wa Mara una tatizo la kukwama kwa miradi mfano mzuri ni ile hospitali ya Mwalimu Nyerere iliyoanza kujengwa miaka ya 70 hadi Serikali ya awamu ya tano ilipoanza kutoa fedha kwaajili ya kuikwamua" amesema na kuongeza

Mradi mwingine nimeambiwa ni huo wa unwagiliaji wa  Bugwema ambao na wenyewe nao umekwama kuanzia mwaka 1970 lakini niwaambie tunakwenda kufanyia kazi.

Amesema kuwa suluhisho la tatizo hilo atalitoa kwa manufaa ya wananchi na kwamba hali hiyo haikubaliki huku akisema kuwa inasikitisha kuona miradi ikikwama wakati wapo viongozi kuanzia ngazi ya mkoa hadi wilaya.

Rais Samia ameweka jiwe la msingi kwenye mradi wa maji wa Mugango-Kiabakari mradi unaotarajiwa kugharimu zaidi ya Sh70.5 bilioni hadi kukamilika.

Amesema kuwa mradi huo awali ulikuwa utekelezwe kwa awamu mbili lakini baadaye aliagiza Wizara ya Maji kuutekeleza kwa awamu moja kwani uwezo w akufanya hivyo ulikuwepo.

Amesema kuwa baada ya kubaini kuwa mkandarasi wa awali aliyepewa kazi ya kutekeleza mradi huo hakuwa na uwezo huo aliagiza wizara imuondoe na atafutwe mkandarasi mwingine.

"Alipatikana mkandarasi akawa na figisufigisu nikaagiza aondolewe nashukuru Wizara ya Maji mlifanya hivyo na kazi inaendelea niwahakikishie kuwa mradi utakamilika kama ilivyopangwa "amesema Rais Samia

Awali akizungumzia mradi huo, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alisema kuwa mradi huo utakuwa na uwezo wa kuzalisha ziada ya mahitaji ya maji katika vijivi 39 vinayoenda kunufauka ambapo mahitaji ni lita milioni 12 lakini mradi huo utakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 35.

Aweso amesema kuwa Wizara ya Maji haitakuwa kikwazo cha lengo la Serikali la kuhakiksiha kuwa wananchi wanapata maji safi na salama.

"Mheshimiwa Rais nikuambie tu kuwa kuchezea miradi ya maji ilishakuwa hadithi za zilipendwa na kila siku nawaambia watendaji wa wizara ya maji kuwa ukishiba chezea kidevu chako na si miradi ya maji na kweli namaanisha" amesema Aweso.

Amesema kuwa wizara ya maji iliamua kuvunja mkataba na mkandarasi wa awali aliyetakiwa kutekeleza mkataba huo baada ya kubaini kuwa ana mapungufu na asingeweza kutekeleza au kuukamilisha mradi huo.


Post a Comment

0 Comments