Safari za Rais kimataifa na faida zake katika diplomasia ya uchumi duniani

 Kati ya mambo yanayotiliwa mkazo na Serikali ni kukuza diplomasia ya uchumi. Pamoja na mambo mengine, wanadiplomasia wa Tanzania nje ya nchi wanategemewa kukuza diplomasia ya uchumi.

Utendaji wa mabalozi wa Tanzania unapimwa kwa namna wanavyotekeleza dhana hii. Kati ya mambo ambayo Rais Samia Suluhu Hassan anayasisitiza ni diplomasia ya uchumi na yeye mwenyewe amekuwa akisafiri nje kuhamasisha na kutekeleza hilo kwa vitendo.


waka mmoja sasa tangu aapishwe kuiongoza Serikali, Rais ameshaenda Kenya, Uganda na Rwanda mwaka 2021 kisha Ufaransa na Ubelgiji mwaka huu. Katika kipindi hicho, ameshahutubia mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa pia.

Kati ya masuala anayofanya Rais katika ziara hizi ni kukutana na mamlaka na jumuiya ya wawekezaji na wafanyabiashara wa anakotembelea.

Wawakilishi wa Tanzania nchi za nje wakiwamo mabalozi hufanya shughuli nyingi zikiwamo za kisiasa, kijamii, kijeshi, kibiashara na kiuchumi. Dhana ya diplomasia ya uchumi inajielekeza kwenye uwekezaji na biashara.

Kila nchi hujihusisha kiuchumi na mataifa mengine kwa kuzingatia mambo ya msingi yanayojumuisha kuvutia wawekezaji, kukuza biashara na kuimarisha ushirikiano.

Kuvutia uwekezaji

Kati ya mambo ya msingi katika diplomasia ya uchumi ni kuvutia uwekezaji kutoka nchi nyingine. Kuna mambo ya msingi ya kuzingatia kufanikisha hili ukiwamo ujuzi maalumu.

Ni muhimu kujua fursa za uwekezaji zilizopo katika nchi na miradi inayoweza kutekelezwa. Fursa na miradi hii inapaswa kubainishwa katika mikoa na wilaya zote na maeneo ya kipaumbele.

Ni muhimu kujua malengo, sera na mipango ya nchi katika uwekezaji. Vilevile ni lazima kujua taratibu zinazotakiwa kufuatwa katika sekta na mradi mmojammoja. Ni muhimu kujua vivutio vya uwekezaji vinavyotolewa na nchi na namna ya kuvipata.

Ni muhimu pia kujua wawekezaji wanataka nini kabla hawajafanya uamuzi ili kurahisisha juhudi za kuwavutia. Wakishakuja, kuwe na mkakati wa kuhakikisha wanaendelea kuwepo. Wanaotekeleza diplomasia ya uchumi wanatakiwa kuyajua yote haya na namna ya kuyatekeleza inavyotakiwa.

Kukuza biashara

Diplomasia ya uchumi pia inahusisha shughuli za biashara. Kati ya mambo muhimu ya kipaumbele ni kuwezesha biashara na nchi za nje ifanyike kwa urahisi ikiwamo kununua na kuuza bidhaa na huduma kati ya nchi husika.

Diplomasia ya uchumi inapaswa kuwezesha wafanyabiashara kupata masoko ya huduma na bidhaa wanazozalisha wakitaka kuuza katika masoko ya nje. Katika jambo hili wanapaswa kuonyesha ukubwa wa soko la bidhaa na huduma husika na taratibu za kuingia katika masoko hayo.

Pamoja na kuwezesha uuzaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi, diplomasia ya uchumi inapaswa kuwezesha ununuzi wa bidhaa na huduma kutoka nje kuja Tanzania. Hii ni pamoja na kuzibaidi bidhaa na huduma, bei na taratibu za kuzinunua ili kuzitumia Tanzania.

Pamoja na hili, diplomasia ya uchumi inapaswa kuwawezesha wafanyabiashara wa Tanzania kushiriki katika mikutano, makongamano na maonyesho ya biashara katika nchi walizopo. Vilevile wanapaswa kusababisha wafanyabiashara kutoka katika nchi walizopo kuhudhuria katika mikutano, makongamano na maonyesho ya biashara yanayofanyika Tanzania yakiwamo ya Sabasaba na Nanenane.

Kukuza utalii na ujuzi

Katika diplomasia ya uchumi, kuvutia watalii kutoka nje kuja nchini ni jambo muhimu. Kama ilivyo kwa uwekezaji na biashara, wanadiplomasia wetu wanapaswa kuwa wawezeshaji wa kuwaleta watalii nchini.

Kwa mantiki iliyotumika katika uwekezaji na biashara, lazima wajue mambo yote muhimu kuhusu vivutio vya utalii vilivyopo nchini na gharama zake. Wanatakiwa kutangaza na kujibu maswali ya wanaotaka kutalii Tanzania kuhusu namna ya kufika na taarifa za kila kivutio cha utalii.

Kusudi diplomasia ya uchumi ifanyike vizuri, kwa ufasaha, ufanisi na jinsi inavyotakiwa, ujuzi wa wanadiplomasia ni muhimu sana. Hii ni kwa mwanadiplomasia mkuu kama vile balozi na timu yake yote.

Kimsingi, diplomasia ya uchumi ni juu ya uchumi kuliko diplomasia tu. Kwa mantiki hii ni lazima wanadilomasia wafahamu vizuri na kuwa na weledi sio kuhusu diplomasia tu bali uchumi. Hata kama uchumi sio kitu wanachokifahamu vizuri zaidi, ni ujuzi wa lazima katika kazi ya diplomasia ya uchumi.

Uzuri ni kuwa kila mara kuna nafasi ya kujifunza kile tusichofahamu kama nchi na zaidi kwa mtu mmojammoja wakiwemo wanadiplomasia.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments