Recent-Post

Shahidi katika Kesi ya Paul Gicheru mahakama ya ICC amhusisha William Ruto na kutoa hongo

William Ruto

Shahidi katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) amelipua bomu baada ya kumhusisha Naibu Rais wa Kenya, William Ruto na kashfa ya kutoa hongo katika njama za kuvuruga kesi ya uhalifu dhidi ya binadamu baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.

Shahidi huyo aliyetambulishwa kama P-0341 alitoa madai hayo jana Jumatatu, Januari 21, wakati wa kesi ya wakili Mkenya, Paul Gicheru katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu huko Hague nchini Uholanzi.

Wakili Paul Gicheru anakabiliwa na mashtaka ya kuwashawishi mashahidi kwa kutumia hongo wakati wa kesi ya Ruto na mwanahabari wa redio, Joshua Sang, katika mahakama hiyo, na kusababisha kusambaratika kwa kesi za uhalifu dhidi ya binadamu zinazowakabili.

 Mashtaka yanayomkabili Gicheru ni pamoja na kukiuka taratibu za kesi, kuwatishia, kuwaua na kutoa hongo kwa mashahidi ili kutatiza mchakato wa kesi.

Shahidi P-0341, ambaye ni wa pili wa upande wa mashtaka katika kesi ya Gicheru, amesema pesa za hongo alizopewa zilitoka moja kwa moja na ziliidhinishwa na Naibu Rais wa Kenya William Ruto.

Shahidi huyo amesema alidai shilingi milioni 20, shamba, gari na kazi kwa ajili ya watoto wake ili kutupilia mbali mpango wake wa kutoa ushahidi dhidi ya Ruto. Amesema Ruto aliidhinisha shilingi milioni 2 pekee na matakwa yake mengine. 

"William Ruto ndiye aliyeidhinisha matakwa yangu. Gicheru aliniambia kuwa Ruto ameidhinisha pesa hizo na vitu vingine nilivyopaswa kupewa", amesema shahidi P-0341.


 Katika habari nyingine, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu imefichua utambulisho wa "mtu mkubwa" ambaye alitoa hongo kubwa kwa mashahidi katika kesi ya Ruto kwenye mahakama hiyo.

Wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo, upande wa mashtaka umewasilisha maoni ya mashahidi waliofichua kwamba "mtu mkubwa" aliyetoa hongo ya shilingi milioni 1.5 ili wajiondoe kwenye kesi hiyo ni William Ruto.

Ushaidi huo unamtia matatani Naibu Rais wa Kenya, William Ruto hususan katika kipindi hiki cha joto la kisiasa la kipindi cha kuelekea kwenye uchaguzi wa rais mwishoni mwa mwaka huu.  

Post a Comment

0 Comments