Recent-Post

Siku 202 za Mbowe jela, hatima yake


Zikiwa zimetimia siku 202 tangu kesi ya ugaidi inayomkabili Freeman Mbowe na wenzake watatu ianze katika Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi Agosti 31, 2021, leo ndiyo itajulikana kama washtakiwa hao wana kesi ya kujibu au hawana.

Hatua hiyo inakuja baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wake kwa kuwaita mahakamani mashahidi 13 kati ya 24 iliokuwa imepanga kuwaita, huku ikitoa vielelezo 39.

Tangu kesi hiyo ianze, imesikilizwa na majaji watatu -- Elinaza Luvanda, Mustapher Siyani na Joachim Tiganga.

Kwa upande wa Jamhuri, mawakili ni Robert Kidando, Pius Hilla, Abdallah Chavula, Jenitreza Kitali, Nassoro Katuga, Esther Martin, Tulimanywa Majige na Ignasi Mwinuka.

Upande wa utetezi wamekuwa na jumla ya mawakili 26 wakiongozwa na Peter Kibatala, baadhi yao ni Nashon Nkungu, John Mallya, Dickson Matata, Fredrick Kihwelo, Faraji Mangula, Sisty Aloyce, Michael Mwangasa, Gaston Garubindi, Seleman Matauka, Maria Mushi, Hadija Aron, Idd Msawanga.

Agosti 23 2021, walifikishwa tena Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Mbowe akasomewa mashtaka hayo ya Uhujumu Uchumi na ugaidi ndani yake.

Alisomewa maelezo ya mashtaka matatu, kufadhili vitendo vya ugaidi na kula njama na kusabisha majeraha kwa aliyekuwa mkuu wa Wilaya Hai, Lengai Ole Sabaya.

Mahakama hiyo ilielezwa na upande wa mashtaka kuwa mshtakiwa namba nne, Mbowe, katika kesi hiyo alikataa kutoa maelezo yake polisi badala yake alisema atayatoa mahakamani.

Upande wa mashtaka ulisema unatarajia kuwa na mashahidi 24 akiwamo aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi (DCI), Robert Boaz na vielelezo vya maandishi 19 huku upande wa utetezi ukiweka wazi mashahidi wake wawili -- IGP Simon Sirro na Ole Sabaya na kuwa wengine wangetajwa baadaye.

Agosti 31, 2021 Mbowe na wenzake watatu walifikishwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kwa ajili ya kuanza usikilizaji wake.

Mawakili wa utetezi wakiongozwa na Kibatala waliiambia mahakama hiyo kuwa, haina mamlaka ya kisheria kuisikiliza kesi hiyo na Jaji alilazimika kuiahirisha hadi siku iliyofuata, Septemba 1, 2021 ili kutoa maamuzi.

Septemba 1 2021, Jaji huyo alitupilia mbali pingamizi la Mbowe na wenzake. Hivyo kesi hiyo iliendelea kusikilizwa mahakamani hapo. Kesi iliahirishwa hadi Septemba 3, 2021.

Septemba 6, 2021 Jaji Elinazer Luvanda alitangaza kujitoa kuisikiliza kesi hiyo baada ya washtakiwa hao kuieleza Mahakama hawana imani naye. Kesi iliahirishwa hadi Septemba 8, 2021 alipopangiwa Jaji Mustapha Siyani.

Oktoba 8, 2021 Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alifanya uteuzi wa viongozi mbalimbali akiwamo Jaji Mustapha Siyani aliyeteuliwa kuwa Jaji Kiongozi.

Oktoba 20 2021, Jaji Siyani alitupilia mbali mapingamizi mawili yaliyowekwa na upande wa utetezi katika kesi ya Mbowe na wenzake, kupinga maelezo ya onyo ya mshtakiwa Adam waliyodai yalichukuliwa nje ya muda na yalichukuliwa baadaye ya kuteswa. Kisha jaji huyo akajitoa katika kesi kufuatia majukumu yake mapya.

Oktoba 26, 2021, baada ya kesi kusimama kwa siku saba kufuatia kujitoa kwa Jaji Kiongozi Siyani, ilijulikana kuwa Jaji Joachim Tiganga ndiye amepangiwa kesi hiyo.

Baada ya hatua hiyo mahakama iliendelea kuwasikiliza mashahidi kuanzia wa kwanza hadi wa 13.

Februari 15 mwaka huu, shahidi wa 13 wa mashtaka, Mkaguzi wa Polisi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi, Mkoa wa Kipolisi Temeke, Tumaini Swila alimaliza kutoa ushahidi wake baada ya kuhojiwa maswali ya dodoso na upande wa utetezi.

Baada ya shahidi huyo kuhitimisha ushahidi wake, Wakili wa Serikali Robert Kidando aliiambia Mahakama Kuu kuwa wamefunga ushahidi na kuiomba Mahakama iwaone washtakiwa wote kuwa wana kesi ya kujibu.

Wengine waliotoa ushahidi wao ni Kamanda wa Polisi wa Kinondoni (RPC), Ramadhani Kingai ambaye alipanda kizimbani Septemba 15, 2021 na kumaliza Oktoba 27, 2021 akifuatiwa na Mkaguzi wa Polisi, Mahita Omary Mahita Novemba 5, 2021.

Wengine ni Walerian Mtaro, Frank Kapalo, Sebastian Madembwe, F. 5614: D/CPL Hafidhi na wa nane ni Mrakibu wa Polisi (SP) Jumanne Malangahe.

Januari 14 mwaka huu, shahidi wa tisa kwa upande wa Jamhuri, Gladys Fimbari, ambaye ni mwanasheria wa kampuni ya Airtel, alimaliza kutoa ushahidi wake.

Shahidi wa 10 alikuwa ni Inspekta Innocent Ndowo ambaye Januari 17 mwaka huu aliugua ghafla wakati akiendelea kutoa ushahidi na kusababisha kuahirishwa kwa kesi hiyo.

Januari 24 ilikuwa ni zamu ya shahidi wa 11 Jamhuri, Goodluck Minja, ambaye aliyeshiriki hatua zote za ukamataji wa washtakiwa katika kesi hiyo.

Shahidi wa 12 alikuwa Ofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Dennis Urio kutoka Kikosi 92 KJ cha Ngerengere, Morogoro cha makomandoo. Mkaguzi wa Polisi, Tumaini Swila alikuwa shahidi wa 13 na wa mwisho kwa upande wa Jamhuri. Februari 9 mwaka huu, Swila alishindwa kuendelea kutoa ushaidi, hivyo kesi hiyo kushindwa kuendelea baada ya shahidi huyo kuanza kujisikia vibaya akiwa kizimbani.

Hata hivyo, ilipofika Februari 14 aliendelea na ushahidi wake hadi alipomaliza Februari 15.

Baada ya kumaliza kumhoji shahidi wa 13, Wakili wa Serikali, Robert Kidando alisema, “Mheshimiwa Jaji baada ya shahidi huyu namba 13, tumefanya ‘assessment’ (tathmini) ya kesi yetu kwa maana ya ushahidi ambao umetolewa mpaka sasa.

“Ni maoni yetu kwamba tume ‘discharge burden’ tunayotakiwa kisheria, hivyo tunaialika Mahakama yako tukufu chini ya kifungu cha 41 (1) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Rushwa ya 2019 ione kwamba washtakiwa wote wanne wana kesi ya kujibu.

Baada ya kusema hayo, kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Peter Kibatala aliomba upande wa utetezi kutoa maelezo ya kutokuwa kesi ya kujibu na aliomba watoe wasilisho la mdomo.”

Baada ya majadiliano ya faragha kati ya Jaji Tiganga na mawakili wa pande zote mbili, Jaji alisema: “Mahakama itapitia ushahidi wa upande wa mashtaka (kuona) iwapo washtakiwa watakuwa na kesi ya kujibu au hapana, Februari 18, 2022.

Post a Comment

0 Comments