Simba wavunja ukimya mkataba wa GSM

SAKATA la Kampuni ya GSM kujiondoa katika udhamini mwenza wa Ligi Kuu Bara limechukua sura mpya baada ya klabu ya Simba ambayo inatajwa kuhusika kuweka msimamo huku wanasheria nchini wakieleza kwa maelezo ya GSM inaonyesha kuna udhaifu kwa upande wa Shirikisho la Soka nchini (TFF).

Juzi, Ofisa Biashara wa GSM, Allan Chonjo alisema wamejiondoa kwenye udhamini huo wa ligi baada ya TFF na Bodi ya Ligi kushindwa kusimamia makubaliano yaliyopo kwenye mkataba walioingia Novemba mwaka jana.

Mwananchi imedokezwa, fedha za udhamini zilipaswa kuanza kutolewa Januari mwaka huu lakini baada ya kuonekana kuna vipengele vya kimkataba vinakiukwa, GSM walisimamisha zoezi hilo kabla ya kutangaza kujiondoa juzi huku klabu ya Simba ikitajwa kuhusika.

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mulamu Nghambi alisema licha ya wao kutajwa kuhusika katika barua iliyotolewa, lakini kama viongozi wataendelea kusimamia msimamo ambao ulilenga kutaka uwazi juu ya makubaliano yaliyopo baina ya GSM na TFF.

“Kujitoa kwao hatuwezi kusema sisi tuko sahihi au laah! lakini itoshe kusema hilo liko juu yao nasi tutabaki na msimamo wetu kwenye jambo lolote, maana hatuwezi kuingia mikataba ambayo hatujui klabu yetu itanufaika na nini hasa,” alisema Mulamu

Wakizungumzia sakata hilo zikiwa zimepita siku 76 tangu mkataba huo wa miaka miwili wenye thamani ya Sh2.1 bilioni uliposainiwa Novemba mwaka jana, baadhi ya wanasheria nchini walisema kila mkataba una njia ya kuingia na kutoka na ndivyo ulikuwa huo wa GSM.

Wakili Frank Chacha alisema kwa namna moja au nyingine kumeonekana na udhaifu upande wa TFF kutokana na maelezo ya barua ya GSM.

“Hatufahamu kiini cha mkataba, lakini kwa barua ya GSM kama ni kweli, basi inaonyesha kuna udhaifu upande wa TFF na Bodi ya Ligi,” alisema.

Ingawa TFF na Bodi ya Ligi jana walipotafutwa walikataa kuzungumzia sakata hilo, Chacha alisema Simba ilikataa kutii matakwa ya mkataba huo kwa kuvaa nembo ya mdhamini mwenza na TFF ilishindwa kuibana klabu hiyo.

“Mdhamini mwenza ni kama hakupewa mazingira rafiki na nembo zake kushindwa kuheshimiwa na baadhi ya klabu, pia kwa nini TFF ilidhamini mkataba bila mdhamini kuweka kianzio?” alihoji.

Alisema kingine kinacholeta ukakasi ni klabu nyingine 15 ambazo zilitimiza masharti ya mkataba, wametekeleza na hawajapata haki.

Awali klabu nyingi za Ligi Kuu zilifichua kwamba katika mkataba wa GSM na TFF bado hawajapata pesa yoyote, ingawa habari zaidi zinadai zipo klabu ambazo zimepata, lakini TFF wala Bodi ya Ligi hawakutaka kuweka wazi juu ya hilo.

“TFF kama mwakilishi wao kwenye mkataba huo anapaswa kuzilipa klabu kwa kile walichotangaza kipindi chote tangu mkataba kusainiwa kwa kuwa zinapaswa kunufaika tangu mkataba uliposainiwa,” alisema.

Wakili mwingine wa kujitegemea, Kasanda Mitungo alisema japo mkataba ulikuwa ni wa Bodi, TFF na GSM, lakini klabu kama wadau wa mkataba ule zilipaswa kuufahamu.

“Ilizuia mtu yoyote kuhoji, lakini klabu zilipaswa kufahamu na sintofahamu ilianzia kwa Simba kukataa kuvaa nembo ya mdhamini mwenza huyo kwa madai kwamba hawakushirikishwa.

“Kwa maelezo ya barua ya GSM, inaonyesha TFF na Bodi ya Ligi ndiyo wamevunja mkataba huo kwa kutotimiza makubaliano na GSM yenyewe imeusitisha.

“Kisheria ni sahihi, japo hatujui kitu gani ambacho TFF na Bodi hawakuvitimiza kwa kuwa mkataba huo hatujauona na ni sahihi TFF kutuonyesha, lakini klabu zote 16 zilipaswa kuufahamu,” alisema Mitungo.

Alisema sheria ya mkataba inatoa nafuu kwa mtu aliyeumizwa na upande mwingine katika masuala ya kimkataba na kubainisha kwamba kipimo cha mkataba ni utekelezaji na uwajibikaji.

“Kama kile ambacho GSM anakisema ni kweli basi ni haki yao kusitisha na kwenye hilo waliovunja mkataba ni wale walioshindwa kutimiza majukumu na sheria inaruhusu kudai fidia kutegemea na mkataba wao unasema vipi, kama hausemi, basi wanaweza kufungua shauri la kudai fidia,” alisema.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments