SINTOFAHAMU YA KADI ZA CCM YAIBUKA BABATI

Sintofahamu imeibuka kwa baadhi ya wanachama wa CCM wa Wilaya ya Babati Mjini Mkoani Manyara, wakilalamikia utaratibu wa ugawaji wa kadi za chama hicho kwa manufaa ya watu wanaotaka madaraka kwenye uchaguzi mkuu wa CCM unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

Wanachama hao ambao waligoma kutaja majina yao wakizungumza jana mjini Babati wameomba viongozi wa CCM wa mkoa huo kuingilia kati na kuchukua hatua ili ugawaji huo wa kadi usiofuata utaratibu ukomeshwe.

Mmoja kati ya wanachama hao amedai kuwa watu hao wamepata kadi hizo na wanatarajia kuzigawa kuanzia mwezi ujao wa Machi kwa watu wao ili waweze kuwaingiza madarakani.

Kadi zinapaswa kutolewa kwenye na tawi kugongwa muhuri na kuingizwa kwenye rejesta ya chama ila katibu tawi ndiyo anapaswa kuainisha mahitaji yake ya kadi kwa katibu kata akiambatanisha orodha ya waombaji wa kadi na siyo kama kama ilivyo sasa kwa kadi kupokelewa kutoka juu bila barua ya maombi ya katibu wa wilaya,” amesema.

Mmoja kati ya wanachama wa chama hicho kwenye kata ya Maisaka alisema Mwenyekiti wa CCM wa kata moja alikuwa na kadi 300 anazogawa kwa watu wake bila utaratibu.

Huyu Mwenyekiti alikuwa na kadi hizo tangu mwezi Desemba mwaka jana na alikuwa anagawa kwenye mfumo usio rasmi kwa watu ambao hawajaomba kupitia ofisi ya tawi lolote lile ila bado yupo nazo nyingi akisubiri mwezi Machi,” amesema.

Mwanachama mwingine amesema miongoni mwa wanaogawa kadi hizo za mchongo ni kiongozi mmoja Mwenyekiti wa Serikali ya mtaaa uliopo kata ya Bagara mwenye kadi 700.

Amesema kadi ya CCM inapaswa kugongwa muhuri na katibu wa Tawi ila Mwenyekiti huyo wa Serikali amekuwa anagawa kadi hizo za mchongo kwa wanachama wapya bila kufuata utaratibu halali.

Mwenyekiti mstaafu wa halmashauri ya mji wa Babati Mohamed Farah maarufu kama (Mwanamaombi) amesema hata yeye alisikia taarifa za kuwepo kadi zinazogawanywa kwa watu bila utaratibu.

Farah amesema endapo utaratibu huo utatumika utakiharibu chama chao, kwanza unachangia kuwafanya wanachama kutokuwa na mazoea ya ulipaji wa ada na kukaa kusubiri uchaguzi na utaratibu huu pia ndiyo chanzo cha kupata viongozi wabovu wasio na sifa ndani na nje ya chama.

Pengine ungezungumza na katibu wa CCM wa wilaya ya Babati mjini ambaye ndiye mtendaji mkuu wa chama kwenye eneo hili, anaweza kukueleza zaidi juu ya hilo,” amesema Farah.  

Katibu wa CCM wa wilaya ya Babati mjini Daniel Muhina amekiri kuwa na kadi mpya ambazo zipo ofisini kwake na amezipokea kwa utaratibu kutoka ofisi ya CCM mkoa wa Manyara.

Amesema kadi zote ambazo zipo kwenye matawi na zinagawiwa hivi sasa kwa wanachama wapya ni halali na makatibu wa matawi waliozichukuwa walisaini kabla ya kupatiwa.

Hakuna kadi ambazo zinagawiwa mitaani bila utaratibu ila ni uzushi tuu kwa baadhi ya watu wenye lengo la siasa za kuchafuana ndiyo wanazungumza hayo,” amesema Muhina.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments