Taasisi yatoa mafunzo ya ujenzi wa barabara kwa teknolojia rahisi


Wanafunzi wa kozi fupi ya matengenezo na ukarabati wa barabara kwa kutumia teknolojia ya nguvu kazi na mitambo mepesi wameanza ukarabati wa barabara ya Veta-Morogoro Hoteli yenye urefu wa mita 350 ikiwa ni sehemu ya mafunzo kwa vitendo mkoani hapa.

Akizungumza na Mwananchi leo Februari 23 mjini, mkufunzi wa kozi hiyo kutoka taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi tawi la Mbeya, Donatha Kamwela amesema, wanafunzi hao watapata kozi fupi ya namna ya ukarabati na ujenzi wa barabara.

Donatha amesema kuwa programu ya kozi hiyo imelenga kuwafundisha wanafunzi njia rahisi za kukarabati barabara na ujenzi na baada ya kufuzu watakuwa na sifa ya kuajiriwa katika katika miradi ya ujenzi ya halmashauri.

“Taasisi hii ya Teknolojia ya Ujenzi inatoa mafunzo ya matengenezo na ukarabati wa barabara kwa kutumia teknolojia ya nguvu kazi na mitambo myepesi kwa vijana ili wapate ujuzi wa kutengeneza na kukarabati barabara za mitaa ndani ya halmashauri,” amesema Donatha.

Baadhi ya wanafunzi wa kozi hiyo, Angelina Gerald na Genovefa Barnabas wamesema mafunzo hayo kwa vitendo yamewapa mwanga katika utengenezaji wa barabara na kukarabati, kusimamia vibarua na kujifunza namna ya kuandaa mikataba kwa urahisi.

Angelina amesema mafunzo hayo yatakuja kuwasaidia siku za usoni kwa wanafunzi hao kuunda vikundi vidogo vidogo vitakavyokuwa na uwezo wa kukarabati miundombinu ya barabara kwa kutumia teknolojia rahisi.

Genovefa ameongeza kwa kusema, “Tunajifunza namna ya kukarabati barabara kutumia vifaa rahisi badala ya kutumia mitambo mikubwa na kazi kubwa ni nguvu kazi ya watu na mikono na vifaa vinavyotumika kamba kwa ajili ya kupimia vipimo mbalimbali, miti, sepetu, majembe na mtambo mdogo wa kushindilia.”

Naye Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi Morogoro, Alfred Jumanne amesema wanafunzi hao wanashiriki ukarabati huo kwa vitendo baada ya taasisi hiyo kuomba barabara hiyo kutumika kujifunzia kwa ujenzi wa kiwango cha changarawe.

“Barabara hii ina urefu wa mita 350 ya Veta-Morogoro Hoteli imekuwa ikisahaulika miaka na miaka katika kukarabati na sisi tulivyokuja na hii kozi tutawatumia zaidi wananchi wa eneo husika na wanafunzi wetu kujifunza kukarabati hizi barabara,”amesema Alfred.

Alfred amesema barabara nyingi zinazoharibika zinatokana na maji kupita katikati ya barabara baada ya kukosa sehemu ya kupita ambayo ni mifereji na wao wamekuwa wakiwafundisha wanafunzi hao njia za kulinda barabara.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments