Tangu Bernard Morrison alipoenda kwenye kibendera kukatika akishangalia bao la kusawazisha la Simba dhidi ya ‘Wanija’ wa US Gendarmerie, ilimaanisha Simba wamepanda kileleni mwa kundi D, huku wakiwaacha USG wakijitafuta kusini kabisa mwa kundi.
Bernard Morrison! Bingwa wa kukera na kuwafurahisha watu wake wa Simba. Wiki iliyopita, niliandika hapa juu ya nidhamu ya Morrison na jinsi alivokuwa akiwaudhi mashabiki wa Simba.
Ni baada ya kutoroka kambini na kusimamishwa na uongozi wa klabu. Alisamehewa kama ambavyo nilitabiri na wiki moja mbele alikuwa akiwafurahisha mashabiki wa Simba.
Morrison alifanya kazi nzuri kuiunganisha kona iliyochongwa kutoka upande wa kulia na kuwapa Simba alama muhimu waliyokuwa wakihitaji ugenini.
Nilijua Morrison atatokea katika sura ya mbele ya kila gazeti la Jumatatu na kila mtu ataisahau kazi ya Shomari Kapombe. Ni kawaida ya soka.
Mara nyingi mfungaji wa bao ndiyo huibuka shujaa wa mchezo. Ni sababu hiyo mpaka leo washambuliaji wanatwaa tuzo za wachezaji bora mbele ya mabeki na viungo.
Hata hivyo bao la Morrison lilianzia kwenye kazi nzuri iliyofanywa katika duara la kona na Kapombe.
Morrison akiwa peke yake katika sanduku, Kapombe alimwona vyema na kukipima kimo chake vizuri kisha akaweka mpira kichwani mwake. Ubora wa lile bao ulitokana na umaridadi wa Kapombe.
Ni bao linalotupa majibu USGN ni timu ya kiwango gani. Si timu ya kiwango cha juu sana kuwazidi Simba.
Kushindwa kumlinda mchezaji ndani ya sanduku lenu mkiwa mnaongoza bao 1-0, ni kosa la kitoto lisilostahili kufanywa katika kiwango cha mashindano ya bara.
Haishtui kusikia hawajawahi kufika hatua ya makundi ya mashindano yoyote Afrika.
Upande wa pili bao lao pia lilitokana na uzembe wa kiungo wa Simba Sadio Kanoute.
Kanoute alikuwa na nafasi nzuri ya kuondoa hatari lakini alitaka kumiliki mpira ulioporwa na mchezaji wa USGN aliyemuona mfungaji vema aliyemtungua Aish Manula aliyekuwa katika kiwango bora sana.
Simba wanaondoka Niger na alama moja kwenda Morocco kuwakabili RS Berkane ambao wakati Simba wanapata sare wao walikuwa wanakufa mabao 3-1 pale Stade de l’Amitie kwa Asec Mimomas.
Hiyo inamaanisha bado timu tatu zina nafasi ya kutoboa kundi D mpaka sasa. Ingekuwa tofauti kama Simba wangekubali kulala dhidi ya USGN.
Simba wataenda Morocco wakijua matokeo ya kupoteza yatawaweka katika hali ngumu bila kujali matokeo yatakayotokea katika mechi ya USGN na ASEC Mimomas.
Kama Simba atakubali kupoteza Morocco, inamaanisha Berkane watapanda juu yao katika msimamo.
Kama mechi ya kule Niger itaisha kwa sare, ASEC watakuwa na alama nne sawa na Simba na kuwasogeza USGN alama mbili nyuma ya Simba.
Kama ASEC atapoteza, USGN atakuwa na alama nne sawa na Simba. Kama ASEC watashinda, watakuwa na alama sita na watakuwa wamepiga hatua mbele ya Simba.
Kumbuka hayo yote ni kama Simba watakubali kupoteza Morocco.
Hiyo ina maanisha, licha ya alama Simba waliyoipata Niger bado wana kazi ya kufanya dhidi ya RS Berkane kule Morocco.
Unaweza kusema Simba wana faida kwa sababu wana mechi mbili nyumbani, lakini kumbuka hakuna tiketi ya moja kwa moja kushinda nyumbani. Ilikuwaje dhidi ya wale makhirikhiri wa Jwaneng? Kumbuka hapohapo kwa Mkapa, Simba alipoteza dhidi ya TP Mazembe Simba day. Kwa vyovote vile, Simba anahitaji alama tatu au moja Morocco.
Simba wataenda Morocco wakijua wana kazi ngumu ya kufanya lakini vichwani mwao watakuwa wakilikumbuka jina la mchezaji wa USGN aliyeitwa Victoria Adebayor.
Ni mshambuliaji msumbufu aliyeipa safu ya ulinzi ya Simba wakati mgumu muda wote wa mchezo. Simba watatamani wasikutane na mshambuliaji wa aina yake tena.
Haitashtua kama jina la Adebayor litaanza kuhusishwa na usajili wa vilabu vya nyumabani.
Simba na Yanga wamekuwa na utaratibu wa kusajili wachezaji waliocheza vizuri dhidi yao au dhidi ya wapinzani wao.
Nasubiri kuanza kusikia Simba na Yanga wakipigana vikumbo kumsajili Adebayor.
0 Comments